Na Esther Mnyika, Dodoma
RAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amemteua Mbunge wa Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Mwigulu ni mwanasiasa mahiri na mtaalamu wa uchumi ambaye safari yake ya kitaaluma na kiuongozi imeanzia katika taaluma ya uchumi hadi kufikia kuteuliwa kushika wadhifa wa Waziri Mkuu.
Alizaliwa Januari 7, 1975 katika Kijiji cha Makunda, Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida.
ELIMU
Mwaka 1987 alianza elimu ya msingi katika shule ya Makunda na kuhitimu mwaka 1993 mkoani Singida. Baadaye alijiunga Shule ya Sekondari Iboru na Mazengo na kuhitimu mwaka 1997.
Mwaka 2004, alipata Shahada ya Kwanza ya Uchumi (Bachelor of Economics) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 2006, alipata Shahada ya Uzamili ya Uchumi kutoka chuo hicho. Mwaka 2018, alipata Shahada ya Uzamivu (PhD) katika uchumi kutoka chuo hicho.
KAZI NA UONGOZI
Kabla ya kuwa Mbunge, Dk. Mwigulu alifanya kazi kama mtaalamu wa uchumi (Economist) Benki Kuu ya Tanzania kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi.Alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Uchumi na Fedha mwaka 2010 hadi 2012.
Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Tanzania kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2013.
Amekuwa Mhazini wa Chama Cha Mapinduzi kuanzia mwaka 2011 hadi 20212.
Amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi kuwanzia mwaka 2012 hadi 2015.
Novemba 2015, aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi hadi mwaka 2016.
Tarehe 11 Juni 2016 hadi 1 Julai 2018 alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani. Mei 2, 2020 hadi 31 Machi 2021, aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Mwaka 2021, Rais Dk. Samia Suluhu alimteua kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ambapo alihudumu nafasi hiyo hadi mwaka 2025.



