📌Mikoa yote nchi nzima kuungwa kwenye Gridi ya Taifa.
Na Mwandishi wetu, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Serikali imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme maradufu hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na mahitaji ya nishati ya umeme nchini.

Akilihutubia Bunge jijini Dodoma Novemba,14 2025 wakati akilifungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia amesema katika kipindi kilichopita, Serikali imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,600 hadi zaidi ya megawati 4,000, hatua iliyowezesha vijiji vyote nchini kufikiwa na miundombinu ya umeme.
“Tunapoelekea mwaka 2030, tumejiwekea lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme maradufu na kupanua mtandao wa umeme ili kufikia vitongoji vyote nchini,”amesema.
Amebainisha kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo nyingi za nishati ikiwemo maji, jua, gesi, jotoardhi, upepo na hata nguvu ya nyuklia ambavyo vyote wanakusudia vitumike katika kuchangia kuongeza nguvu kwenye uzalishaji wa umeme nchini kuendelea kuwa wa uhakika na endelevu.
Kupitia Mpango wa Gridi Imara,amesema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme na itaendelea kuongeza vituo vya kupoza umeme nchini ili kuongeza nguvu ya umeme kwa matumizi ya viwanda, biashara na makazi.
Rais Samia pia ametaja kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, mikoa yote ya Tanzania inakuwa imeunganishwa na Gridi ya Taifa.



