📌Asema siku mia moja za Rais ni dira ya kufikia malengo
📌Asisitiza ushirikiano baina ya watumishi na viongozi ndani ya Wizara ya Nishati
Na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nishati Deogratius Ndejembi amewaagiza Watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza Vipaumbele vya Serikali katika Sekta ya Nishati ikiwemo kufikia Megawati 8000 ifikapo 2030.

Ndejembi ameyasema hayo Novemba, 18 2025 wakati akizungumza na watumishi wa Wizara mara baada ya kuwasili Katika Wizara Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Amesema watumishi wa Wizara ya Nishati ndio watendaji wakuu na wenye dhamana ya kuhakikisha kwamba malengo ya Serikali yaliyowekwa yanatimia kwa kufanya kazi kwa bidii , kuwataka watumishi kuchambua kwa kina hotuba ya Mhe Rais ili kuweza kufikia vipaumbele kwa wakati na kuyoa huduma bora kwa wananchi wa Tanzania.

Pia amesisitiza watumishi kutumia siku mia moja za Rais kama kipimo na kielelezo cha kutathmini uelekeo wa malengo ya Serikali.
“Sisi kama viongozi wenu tunategemea zaidi ushirikano kutoka kwenu ninyi wataalamu wa hapa Wizara ya Nishati ili tuweze kukamilisha Vipaumbele vya Mhe. Rais alivyoviweka katika sekta yetu kwasababu tunatakiwa tuanze kwa kukimbia na sio kutembea,”amesema Ndejembi.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amewataka watumishi kushirikiana kwa pamoja na viongozi wa Wizara hiyo ili kuendesha Sekta ya Nishati kwa pamoja, na kuongeza kuwa anatambua kwamba maswala mengi ya sekta ya Nishati yameshafanyika tayari mpaka sasa.
Amesema Serikali imeshafikisha Megawat 4000 za kiwango cha kuzalisha Umeme, hivyo ni jukumu letu kukamilisha miradi iliyokuwa inaendelea na kuongeza vyanzo vingine vya uzalishaji umeme ili kufikia megawati 8,000 ifikapo 2030.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amewashukuru viongozi hao na amewataka watumishi wa Wizara ya Nishati kutoa ushirikiano kwa viongozi hao sambamba na kutekeleza majukumu yao kwa wakati ili kuweza kutekeleza Vipaumbele vya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ifikapo mwaka 2030.



