Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni mbalimbali zilizofanikisha ukamataji wa jumla ya kilogramu 3,799.22 za dawa za kulevya, kuteketeza ekari 18 za mashamba ya bangi pamoja na kutaifisha mali za wahalifu wa dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi Bilioni tatu na milioni mia tatu na nne (3,304,000,000/=).

Hayo yamebainishwa leo Disemba 3, 2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema watuhumiwa 84 walikamatwa kuhusiana na dawa hizo.
“Katika kuendeleza hatua za kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya, Mahakama kuu divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilitoa maamuzi ya kutaifishwa kwa mali zenye thamani ya Tsh. Bilioni Tatu na milioni mia tatu na nne (3,304,000,000/=) za watuhumiwa Saleh Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Ameeleza kuwa mali hizo zinajumuisha nyumba, viwanja na magari, kwamba maombi ya kutaifishwa kwa mali hizo yaliwasilishwa mahakamani hapo kufuatia uchunguzi uliofanyika na ikabainika kwamba, watuhumiwa hao wanamiliki mali ambazo zilipatikana kwa njia za uhalifu wa biashara ya dawa za kulevya.
Amesema utaifishaji wa mali hizo umefanyika chini ya Sheria ya Mazao ya Uhalifu Sura ya 256 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015.
Amefafanua kuwa utaifishaji wa mazalia ya uhalifu umewekwa kisheria ili kuifundisha jamii kuwa, uhalifu hauna faida na adhabu za kifungo hazitoshelezi kutokomeza uhalifu hasa katika makosa ya kupangwa ikiwemo makosa ya dawa za kulevya. Huu ni mkakati wa kuzuia uhalifu kuendelea na kuondoa matamanio ya kufanya uhalifu.
Ametaja orodha ya mali zilizotaifishwa kuwa ni Apartment Namba OA2, Ghorofa ya Kwanza, iliyopo Sea Breeze Residential Complex, kiwanja Namba 192 Block “O”, Jangwani Beach, Kinondoni, Dar es Salaam.
Mali nyingine ni Apartment 6B, kiwanja Namba 26 Block 52, iliyopo Kariakoo, Ilala, Dar es Salaam, Nyumba iliyo kwenye kiwanja Namba 329 na 1009 Block “C”, Mbezi wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na kiwanja Namba 69 Block 7, kata ya Mbweni JKT, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Amebainisha mali nyingine kuwa ni Nyumba Namba 14, iliyopo kiwanja Namba 131 Block 9, mtaa wa Chui Mtoni Kijichi, NSSF House Scheme Phase III, Temeke, Dar es Salaam, kiwanja Namba 44768, kilichopo mtaa wa Kigogo kata ya Kisarawe II, Kigamboni Dar es Salaam na kiwanja kilichopo Shungubweni Village, kata ya Shungubweni, wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani.
Pia ametaja Kiwanja Namba 53 Block E, Boza Village, Wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani, kiwanja kilichopo Boza village, kata ya Boza wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, kiwanja Namba 8 Block C, kilichopo mtaa wa Mwambao, kata ya mji Mkongwe, wilaya ya Bagamoyo, mkoa wa Pwani na Apartment Namba PA1, Ghorofa ya chini, Sea Breeze Residential Complex, kiwanja Namba 192 Block P, iliyopo Jangwani Beach, Kinondoni Dar es Salaam.
Hakuishia hapo, nyingine ni Nyumba Namba 9, iliyopo Magomeni, wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, kiwanja Namba 44746, kilichopo mtaa wa Kigogo, kata ya Kisarawe II, Kigamboni Dar es Salaam, kiwanja Namba 44748 kilichopo mtaa wa Kigogo, kata ya Kisarawe II Kigamboni Dar es Salaam na kiwanja Namba 44789, kilichopo mtaa wa Kigogo, Kata ya Kisarawe II, Kigamboni Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali Lyimo ametaja Magari yaliyotaifishwa kuwa ni pamoja na, Gari namba T 539 DKQ, Nissan Civilian, Gari namba T 427 EAH, Subaru Impreza, Gari namba T 196 EAC, Volkswagen, Gari namba T 654 DCH, Volkswagen na Gari namba T 141 DKV, Nissan Civilian.
Mengine ni Gari namba T 944 DKY, Nissan Civilian, Gari namba T 830 DLA, Nissan Civilian, Gari namba T 767 DLL, Nissan Civilian, Gari namba T 435 DJY, Toyota Corolla Spacio, Gari namba T 307 DLW, Nissan Civilian na, na Gari namba T 753 DKS, Nissan Civilian.
Kadhalika, amebainisha kuwa Mamlaka hiyo imefanya operesheni mbalimbali Jijini Dar es Salaam ambapo katika eneo la Sinza D, iliwakamata Bw. Cuthbert Kalokola (34) na Bi. Murath Abdallah (19) wakiwa na dawa mpya za kulevya aina ya 3,4 – Methylenedioxymethamphetamine (MDMA) vidonge 738 vyenye uzito wa gramu 177.78 na dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Rohypnol (flunitrazepam) vidonge 24 vyenye uzito wa gramu 10.03.
Kwamba eneo la Mbezi maramba mawili, watuhumiwa Jaribu Tindwa (38), Ally Meshe (39), Juma Mfamo (20) Rahim Nampanda (28), Abubakari Ally (20), Nurdin Rashid (36) na Farid Rashid (33) walikamatwa wakiwa na kilogramu 90 za dawa za kulevya aina ya skanka zikiwa zimefichwa ndani ya matanki ya solar panel zilizokuwa zimepakiwa kwenye basi la Falcon, aina ya Scania lenye namba za usajili T372 DFK linalofanya safari zake kati ya Tanzania na Malawi.
Vilevile, katika operesheni nyingine iliyofanyika Mkoani Rukwa katika mpaka wa Kasesya, alikamatwa Bw. Godwin Andrew (26) mkazi wa Mbalizi Mbeya akiwa na dawa za kulevya aina ya skanka zenye uzito wa kilogramu 244.3.
Amesema Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya spika, mashine za kupooza hewa, mashine za kukatia majani na vifaa vya kompyuta (CPU). Vifaa hivyo vilikuwa vikisafirishwa katika gari aina ya Iveco Van yenye namba za usajili wa nchi ya Afrika Kusini CN 85 FN GP mali ya kampuni ya usafirishaji ya Makamua Logistics Limited lililokuwa likitokea nchini Afrika Kusini kuja Dar es Salaam.
Aidha, katika operesheni zilizofanyika mikoa mingine nchini, zilikamatwa kilogramu 2,041.45 za bangi, kilogramu 1,423.28 za mirungi na ekari 18 za mashamba ya bangi ziliteketezwa. Magari manne na pikipiki 12 vilikamatwa katika operesheni hizo. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa wito kwa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya.



