Home KITAIFA Dk.Migiro: Tunao wajibu kwa Tanzania iliyo salama

Dk.Migiro: Tunao wajibu kwa Tanzania iliyo salama

Na Mwandishi wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Asha Rose Migiro amesema Watanzania wote kwa pamoja, wanaowajibu wa kuhakikisha taifa linakuwa salama kwa kuimarisha misingi na mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Akizungumza leo Desemba , 4 2025, jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Wanawake ambao wamekutana kujadiliana mustakabali chanya wa Tanzania, wakitumia kauli mbiu inayosema “Mama ni Amani.”

“Tumekutana kama kina mama na kauli mbiu yetu inatuambia mama ni amani. Anapokuwepo mama kuna amani kwa namna mbalimbali. Nitumie nafasi hii kuleta salamu kwenu kutoka kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

“Anajua kina mama tunakutana leo, anajua kina baba wataungana nasi leo, anajua vijana wake wako pamoja nasi na taifa hili takwimu zinaonesha vijana ni sehemu kubwa sana ya Taifa letu.

“Kwa hiyo Rais Samia anatoa salamu za pekee kwenu na amefurahi kusikia vijana kuungana mama zenu, baba zenu na walezi wenu katika mada hii muhimu ya mama ni amani,” amesema Balozi Dk. Migiro.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inakwenda sambamba sambamba na falsafa ya Rais Samia ya mambo manne, ambapo mojawapo ni ustahimilivu. Akisema kuwa, pamoja na changamoto zilizojitokeza, bado nchi yetu imesimama imara.

“Na kupitia yale ambayo tumeona na Rais ameyaeleza nchi yetu iko tayari kujenga upya, nchi iko tayari kuimarisha yale mazuri na ndio maana jukwaa letu leo limewaleta wanawake na vijana kwa sababu Tanzania ni yetu sote.

“Sisi wote hatuna pakwenda ila hapa Tanzania kwa mantiki hiyo ujumuishi huu unahakikisha haturudi nyuma. Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan ni mwanamke namba moja, ni kiongozi ni mama, ni mlezi. Leo tunapokaa hapa tunazungunza mchango wa amani katika ujenzi wa Taifa letu,”amesema.

Aidha Katibu Mkuu wa CCM huyo amesisitiza umuhimu wa kuzungumza kwa ajili ya maridhiano, na kwamba huu ni wakati wa Watanzania, wakiwemo wanawake, kuitikio mwito huo kwa kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mazungumzo katika hatua mbalimbali, ikiwemo tume iliyoundwa kuchunguza kiini cha vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here