Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
SERIKALI imeendelea kuimarisha sekta ya nishati kupitia uwekezaji mkubwa wa zaidi ya shilingi trilioni 13.5 katika miradi 41 ya umeme kote nchini huku ikizindua mita janja za umeme kurahisisha utoaji wa huduma kwa Watanzania.

Kati ya miradi hiyo 41, inayohusu uzalishaji ni sita na 35 ni ya usambazaji, hatua ambayo imeelezwa kuwa msingi wa mageuzi ya kiufundi na kiutendaji ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na ukombozi kwa wateja walioteseka na changamoto za umeme kwa miaka mingi.
Akizungumza leo Desemba, 5 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa matumizi ya Mita janja Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi alisema uwekezaji huo mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita unaonesha dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika wa kisasa na unaoendana na kasi ya teknolojia ya sasa.

Amesema Mitajanja ni moja ya matokeo ya uwekezaji huo, ikiwa ni mita za kisasa zenye uwezo wa kutoa taarifa za matumizi kwa muda halisi.
“Mita hizi mpya zinakwenda kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya wateja kuhusu mita za zamani zilizokuwa zikikwama, kupoteza kumbukumbu, kutoa taarifa zisizo sahihi au kuwafanya wananchi kupanda ngazi kila wanapohitaji kuingiza tokeni,”amesema.
Ndejembi amesema mitajanja itamuwezesha mteja kununua umeme akiwa mahali popote pasipo kufika nyumbani, jambo litakalosaidia kupanga bajeti na kufuatilia matumizi kwa urahisi zaidi.

Amesema teknolojia hiyo mpya itaimarisha ukusanyaji mapato ya TANESCO kupitia uwezo wa mita kugundua wizi wa umeme, kubaini hitilafu na kutambua upotevu wa nishati kwa wakati halisi.
“Tunaingia kwenye zama mpya. Sasa TANESCO inaweza kuona matumizi ya umeme kwa usahihi na kudhibiti mianya ya upotevu jambo ambalo litaongeza ufanisi wa shirika,” amesema.
Ndejembi amebainisha kuwa TANESCO tayari imeanza kufunga Mitajanja katika mikoa yote nchini, na maoni ya awali kutoka kwa wateja yamekuwa chanya.
Amesema wateja wapya wanaounganishiwa umeme pamoja na wanaobadilishiwa mita za zamani watapatiwa Mitajanja bila gharama, huku akielekeza hatua hiyo kuharakishwa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kuondoa kabisa matumizi ya mita za zamani.
Pia, amesema TANESCO imewekeza katika mifumo mingine ya kisasa ikiwemo kituo cha kisasa cha huduma kwa wateja (Call Centre) na mfumo wa Chatbot unaomwezesha mteja kujihudumia mwenyewe.
Amesema mifumo hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kidijitali unaolenga kuongeza ufanisi na kupunguza muda wa kushughulikia changamoto za wateja.
Pia amelitaka shirika hilo kuboresha zaidi mawasiliano kwa wateja, hususan wakati wa matengenezo ya miundombinu ambayo mara nyingi hufanywa wakati wananchi wapo majumbani.
Alitaka TANESCO kupanga ratiba rafiki kuepusha usumbufu, akisisitiza kuwa Watanzania wanahitaji umeme wa uhakika wakati wote.

Katika hatua nyingine, ametoa onyo kali kwa matapeli wanaojifanya maofisa wa TANESCO na kuwafuata wananchi kwa madai ya kusambaza au kuuza Mitajanja.
Amesema TANESCO imeweka utaratibu rasmi wa ufungaji wa mita hizo na hakuna mfanyakazi anayepaswa kukusanya fedha au kutembelea wateja bila utaratibu.
“Ninaagiza watakaofanya maboresho ni TANESCO wenyewe, asije akajitokeza mtu na kusema yeye ni TANESCO, Shirika muhakikishwe mita janja ziendane na viwango vya kimataifa vya usalama na ubora,” amesema.
Amewapongeza wataalamu wa ndani ya TANESCO, alisema maendeleo ya mfumo wa Mita janja yamechukua zaidi ya miaka 18 kutengenezwa, na kwamba mafanikio ya sasa ni historia mpya kwa shirika hilo na taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufuatilia hatua kwa hatua hadi Tanzania ifikie mfumo kamili wa usimamizi wa umeme wa kisasa na wa kiuchumi na uwepo wa mita hizo ni hatua inayoashiria mwanzo wa mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za nishati nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amegusia fursa mpya zitakazotokana na teknolojia hiyo, ikiwemo uwezo wa wananchi kuzalisha umeme wa jua katika makazi yao na kuuza ziada itakayobaki kupitia mfumo huo.
Amesema kuwa kupitia mita hizo, mteja ataweza kutumia umeme anaouzalisha na kuuza kiasi kisichohitajika katika gridi, jambo litakalofungua milango ya uchumi na kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati vijijini na mijini.
Ameongeza kuwa mita janja zitaiwezesha TANESCO kubaini maeneo yenye tatizo la umeme bila kusubiri malalamiko ya wateja, kwani mita zitatuma taarifa moja kwa moja mara tu huduma inapokatika.
Kwa upande mwingine, amesisitiza kuwa kuanzishwa kwa teknolojia hiyo kutabadilisha kwa kiwango kikubwa namna TANESCO inavyotoa huduma kwa wateja wake na kuongeza uwazi katika matumizi na usimamizi wa umeme.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,Lazaro Twange alisema mfumo wa mita janja umetengenezwa na wataalamu wazawa wa TANESCO.
“Mita janja zina faida kubwa ikiwa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu, ikiharibika kumbukumbu ya mita inaonekana na mita hizo zina mifumo salama ya udhibiti, haziingiliki kirahisi na kudhibiti mapato,” amesema.



