Home KITAIFA DK. Mwigulu: wafanyabiashara wasinyang’anywe bidhaa zao

DK. Mwigulu: wafanyabiashara wasinyang’anywe bidhaa zao

Na Mwandishi wetu, Dodoma
 
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba ametoa maagizo kwa viongozi wa majiji na halmashauri zote nchini kuhakikisha wafanyabiashara hawanyang’anywi bidhaa zao na badala yake wawaelekeze namna bora ya kufuata taratibu zilizowekwa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Desemba 8, 2025 wakati akizungumza na wafanyabiashara katika soko la Machinga jijini Dodoma baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Richard Joseph ambaye ni mfanyabiashara sokoni hapo aliyedai kuchukuliwa bidhaa zake na watumishi wa jiji.

“Msichukue bidhaa za raia; hizo ndio ofisi za raia wetu, hata kama kuna jambo ambalo anapaswa kuelekezwa kuhusu masuala ya utaratibu basi mshughulikie jambo linalohusu utaratibu, msizuie mitaji ya watu. Utaratibu wa kuchukua bidhaa haukubaliki na hakuna uhalali wa kuchukua bidhaa za raia. Msicheze na mitaji ya watu,” amesema.

Dk. Mwigulu amemuagiza mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule pamoja na Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri wahakikishe wanafuatilia suala hilo na wahusika warudishe bidhaa za mfanyabiashara.  “Kama wamepotea nazo, wachukuliwe hatua kama wezi wengine. Mheshimiwa Rais hapendi uonevu, ni mtu wa haki.”

Waziri Mkuu ambaye amefanya ziara ya kushtukiza sokoni hapo ameagiza wafanyabiashara kutoondolewa kwenye vizimba vyao na kama bado kuna mahitaji makubwa ya maeneo ya kufanyia biashara uongozi wa mkoa utafute maeneo na kujenga masoko ili kutosheleza mahitaji.

Kwa upande wao wafanyabiashara katika soko hilo wamemshukuru Dk. Mwigulu kwa kufanya ziara hiyo ya kushtukiza na kusikiliza kero zao na kumuomba aendeleze utaratibu huo na maeneo mengine ya nchi.

Amewasisitiza Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano ili waweze kufikia malengo ya kimaendeleo yaliyowekwa na Serikali. “Watanzania tukatae kugawanywa.”

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya siku ya Uhuru, Waziri Mkuu amewasihi wananchi kuitumia siku hiyo kwa ajili ya mapumziko isipokuwa kwa wale ambao watalazimika kwenda kazini kutokana na majukumu yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here