Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema vijana wengi bado wamekwama katika fikra za zamani za kutegemea ajira serikalini, akisisitiza kuwa hali hiyo ndiyo chanzo cha kukua kwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa wahitimu nchini.

Akizungumza Leo Disemba, 8 2025 na Waandishi wa Habari jijini Profesa Mkumbo amesema changamoto ya ajira kwa wahitimu inagusa bara zima la Afrika, na Tanzania haiwezi kuendelea kuendeleza mfumo wa kutegemea serikali kuwa mwajiri mkuu wakati nafasi zake ni chache sana na haziwezi kupokea kila mhitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi.
Amesema zama za kuhitimu chuo na kuajiriwa serikalini mara moja ‘zimepitwa na wakati’, na kusisitiza kuwa serikali inachukua hatua mahsusi za kulivunja tatizo hilo kwa kuongeza uwezo wa vijana kujiajiri, kuwekeza na kuajiri wenzao.
Amesema njia pekee ni kuhakikisha sekta binafsi inapanuka na vijana wenyewe kuwa sehemu ya injini ya ajira nchini.
“Miongoni mwa hatua ambazo serikali itazichukua ni kuanzisha Kituo Maalum cha Kuhudumia na Kuwezesha Wawekezaji Vijana (Youth Investors Resource Centre). Kituo hicho kitatoa mafunzo, usaidizi wa uwezeshaji na huduma mbalimbali kwa vijana wanaotaka kuwekeza. Kitakuwa Mabibo, Dar es Salaam, huku kukiwa na uwakilishi katika ofisi za TISEZA za mikoa na kanda,”amesema.
Amesema wanatarajia kukizindua kituo hicho kabla ya mwisho wa mwaka huu.
ProfesaKitila amesema Serikali inaanzisha programu maalum ya kuwezesha vijana kubuni na kuanzisha uwekezaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali nchini. Katika mpango huo, maeneo maalum yametengwa kwa ajili ya vijana waliomaliza vyuo vikuu na vyuo vya ufundi ili waweze kuwekeza.
Serikali imepanga kufanya mageuzi makubwa katika uongozi wa mashirika ya umma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watendaji wakuu na wajumbe wa bodi za wakurugenzi wanapatikana kwa njia ya ushindani ili kuongeza uwazi, uadilifu na ushiriki mpana wa Watanzania wenye sifa.
Amesema mfumo huo mpya utaanza kutumika kuanzia Julai 1, 2026 mara baada ya kupitishwa kwa sheria mpya inayoandaliwa na serikali.
Amesema uamuzi huo ni sehemu ya mpango mpana wa kuboresha utendaji wa mashirika ya umma, kuweka uwazi katika uteuzi wa viongozi, na kuondoa utaratibu wa uteuzi wa moja kwa moja uliokuwa ukilalamikiwa na wadau kwa kukosa ushindani wa wazi.
“Kama ni Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO utaomba, uta-apply, na utashindanishwa. Kama unataka kuwa mjumbe wa bodi ya TPA au TISEZA utapitia mchakato wa ushindani. Watanzania wote wenye sifa wataomba, na uchaguzi utafanywa kwa ‘competitive recruitment,” amesema.
Amesema mageuzi hayo yanakwenda sambamba na hatua kadhaa zinazolenga kuongeza tija ya mashirika ya umma na kuimarisha mchango wake katika uchumi wa taifa na utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Serikali inaunda mfumo mpya na imara wa kupima maendeleo ya mashirika ya umma kwa kuzingatia tija ya kiuchumi na ubora wa huduma. Mashirika hayo yatapewa vigezo vipya vya kupimwa na kila moja litahesabiwa kwa kiwango kinachochangia kwenye uchumi na ustawi wa wananchi,”amesema.
Amesema sheria mpya itayataka baadhi ya mashirika ya umma ya kibiashara kujisajili katika Soko la Hisa ili Watanzania waweze kununua hisa na kumiliki mashirika yao, kupanua uwazi katika uendeshaji, na kuongeza uwajibikaji kwa menejimenti na bodi.



