Home AFYA Kwa pamoja tukaboreshe huduma za afya msingi-Dk.Seif

Kwa pamoja tukaboreshe huduma za afya msingi-Dk.Seif

Na James Mwanamyoto, Dodoma

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Jafar Seif, amewataka viongozi na watumishi wa Idara ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kushirikiana nae katika kuleta mabadiliko yatakayoboresha utoaji wa huduma za afya msingi kwa wananchi katika mikoa na halmashauri nchini.

Dk. Seif ametoa wito huo leo Disemba,10 2025 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chache na watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI (Sokoine) ambacho kililenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa idara hiyo.

“Nahitaji kuona tunabadilika kiutendaji ili kumsaidia Waziri Profesa Mdoe kufikia lengo lake la kuboresha utoaji wa huduma za afya msingi,” amesisitiza Dk. Seif.

Pia ameomba kupewa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake, na kuongeza kuwa katika uongozi wake hategemei kuona watumishi wakishutumiana badala yake wawe na utamaduni wa kuzungumza ili kutatua changamoto zinazowakabili kiutendaji.

“Tunapokabiliana na changamoto, tuzipokee kwa pamoja kama changamoto za idara na tuzitafutie ufumbuzi ili idara isikwame katika kutekeleza majukumu yake,” amehimiza.

Aidha amewakumbusha watumishi wa idara hiyo kutekeleza kikamilifu maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watumishi wa umma wanapeleka tabasamu kwa wananchi kwa kutoa huduma bora.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Profesa Tumaini Nagu amemhakikishia Naibu Waziri Dk. Jafar Seif kuwa watumishi wa wa Idara ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe wako tayari kumpatia ushirikiano utakaomuwezesha kuteleza vema majukumu yake ya Unaibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI (Afya).

Amesema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI inajivunia uwekezaji mkubwa Uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita wa takribani trilioni 1.34 ambazo zimetumika kujenga miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya, ukarabati wa hospitali, pamoja ununuzi wa vifaa tiba ambavyo vimeboresha utoaji wa huduma za afya msingi nchini.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Dk. Rashid Mfaume amesema kuwa, majukumu mahususi ya idara yake ni kufanya ufuatiliaji wezeshi na tathmini kwa kuboresha utawala bora katika utoaji wa huduma za afya, ustawi wa jamii na lishe, ikiwa ni pamoja na kutafsiri miongozo inayohusiana na maendeleo na mkakati wa fedha katika Sekta ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Dkt. Jafar Seif, ameendeleza jitihada zake za kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kada ya afya kwa kufanya kikao kazi na Idara ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI ambayo inajukumu ya kusimamia utoaji wa huduma za afya msingi nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here