Ahimiza matumizi ya mbolea na mbegu za mazao ya muda mfupi
Na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania watunze akiba ya chakula walichonacho na waepuke matumizi yasiyofaa kutokana na hali ya kuchelewa kwa msimu wa mvua.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Desemba 14, 2025) wakati akizungumza na baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
Amewaeleza viongozi hao kutoka mikoa ya Dodoma na Singida kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Desemba 2025 na kipindi cha mwezi Novemba, 2025 hadi Aprili 2026 mtawalia.
“Kutokana na utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.
Amesema tathmini hiyo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaonesha hali ya kuchelewa kwa mvua inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma pamoja na Kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

“Pamoja na kuwa hakuna tishio la uhaba wa chakula kutokana na hifadhi ya chakula iliyopo nchini, lakini ni vema, wananchi waendelee kuzingatia matumizi sahihi ya chakula. Tuna akiba ya chakula ya kutosha lakini ninawasihi wananchi waweke akiba na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wakulima waandae mashamba kwa wakati na watumie pembejeo zinazoendana na upatikanaji wa mvua chache sambamba na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ambao kwa sasa wanazunguka nchi nzima kukutana na wakulima na kutoa elimu.
Vilevile, Dk. Mwigulu amewataka wafugaji wote waweke mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo ili kukabiliana na hali hiyo.
Waziri Mkuu amewasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wahakikishe maafisa ugani wanawatembelea wakulima na kutoa ushauri ikiwemo matumizi sahihi ya mbegu kulingana na hali ya hewa badala ya kukaa ofisini muda wote.
“Vilevile, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri endeleeni kuhamasisha wakulima wajisajili kwenye daftari la mkulima na kuhakikisha wanapata namba za usajili,” amesisitiza.
Amewataka viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) zihakikishe kuwa shehena za pembejeo zinahudumiwa kwa wakati ili usambazaji ufanyike kwa ufanisi.



