Home KITAIFA Dk. Kusiluka awataka Maafisa Habari kuzingatia maadili na weledi ili kulinda maslahi...

Dk. Kusiluka awataka Maafisa Habari kuzingatia maadili na weledi ili kulinda maslahi ya Taifa

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka amewataka Maafisa Habari wa Serikali kuzingatia weledi, maadili na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha mawasiliano ya serikali na wananchi pamoja na kulinda maslahi ya Taifa katika mazingira yenye kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Pia amewataka kutambua kuwa jukumu la Afisa Habari si kumsifu au kumfurahisha kiongozi, bali ni kutoa taarifa sahihi za kazi, mipango na mafanikio ya serikali, sambamba na kukusanya kero za wananchi na kuzifikisha kwa wahusika ili zipatiwe ufumbuzi.

Akizungumza leo Disemba 17,2025 Jijini Dar es salaam Dk. Kusiluka wakati akifungua Kikao Kazi cha Kitaifa cha Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Maafisa Habari wa Serikali,chenye kauli mbiu isemayo “utu na mawasiliano yenye uwjibikaji”

Amesema serikali inawategemea wataalamu hao kama jeshi muhimu katika kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa ufasaha, hususan katika kipindi ambacho taarifa potofu na propaganda zinaweza kutumika kuhatarisha usalama na mshikamano wa nchi.

“kikao hiki kimeandaliwa kwa makusudi ili kuwakutanisha viongozi wapya na wataalamu wa habari mapema, ili kujenga uelewano wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuweka msingi imara wa ushirikiano katika kusukuma mbele ajenda ya serikali,”amesema Balozi Dk Kusiluka.

Amebainisha kuwa teknolojia ya habari imeleta fursa kubwa lakini pia changamoto, huku akionya kuwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yanaweza kuleta madhara makubwa endapo hayatadhibitiwa kwa weledi na uzalendo.

Amewakumbusha Maafisa Habari kuwa wao ni watumishi wa umma walioajiriwa na wananchi, hivyo wanapaswa kutambua kuwa nafasi walizonazo ni dhamana na bahati kubwa inayopaswa kulindwa kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

“Serikali bado haijafanya vizuri vya kutosha katika kuwafikia wananchi kwa taarifa sahihi kuhusu miradi na mipango mikubwa ya maendeleo, hali inayosababisha wananchi kukosa uelewa wa fursa zilizopo na mchango wa serikali katika kuboresha maisha yao,”amesema.

Balozi Dk. Kusiluka amewataka Maafisa Habari kujifunza kwa kina nyaraka muhimu za taifa ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025, akisema humo ndimo kunakopatikana mwelekeo wa sera, miradi na ahadi zinazotekelezwa na serikali, hivyo ni chanzo muhimu cha taarifa kwa wananchi.

“Mshikamano na ushirikiano baina ya Maafisa Habari wa taasisi mbalimbali za serikali, kwani serikali ni moja na inapaswa kuwasiliana kwa sauti moja, badala ya kila taasisi kufanya kazi kivyake kama kisiwa mnapaswa kubadilika,”amesema.

Aidha amebainisha pia umuhimu wa Maafisa Habari kuwa washauri wa kimkakati wa viongozi wao katika masuala ya mawasiliano, kwa kuwa wao ndio wataalamu waliobobea katika tasnia hiyo, hivyo wanapaswa kusimama imara katika kutoa ushauri wa kitaalamu bila woga.

Pia amewahimiza kujiendeleza kitaaluma kwa kujifunza mbinu za kisasa za mawasiliano, kushirikiana na sekta binafsi na kuachana na mtazamo wa kuridhika au kusimama katika maarifa ya zamani.

Ameongeza kuwa Maafisa Habari wa Serikali wako mstari wa mbele katika kujenga umoja wa kitaifa, kulinda amani na kutetea maslahi ya nchi, hivyo wanapaswa kutumia taaluma yao kikamilifu kuhakikisha serikali inawafikia wananchi na dunia kwa ufanisi, uwazi na uaminifu.

Naye Mshauri wa Rais Masuala ya Habari, Tiddo Muhando, amesema dhamira ya Rais ni kuhakikisha anapata taarifa sahihi, zisizoegemea upande mmoja na zinazotoka maeneo yote ya nchi, si Dar es Salaam pekee akisisitiza kuwa taarifa hizo ndizo zitakazomsaidia Rais kuielewa kwa kina hali halisi ya wananchi na maendeleo yanayotekelezwa, hivyo kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bakari Machumu amesema katika dunia ya sasa iliyojaa changamoto na kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa Serikali kuwa mstari wa mbele katika kutoa maelezo ya msingi kuhusu mafanikio inayoyapata.

Amesema kuwa bila kufanya hivyo, Serikali hujikuta ikijibu maswali mengi badala ya kuelekeza mjadala kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.

Ameongeza kuwa matarajio ya kikao kazi hicho ni kutoa fursa ya kubadilishana mawazo, kujifunza na kufahamishana ili kuimarisha namna ya kuwasiliana mafanikio ya Serikali kwa umma wa Tanzania na dunia kwa ujumla. Kwa kufanya hivyo.

Amesema pengo la uelewa kuhusu kazi na juhudi za Serikali litazibwa na kuongeza imani ya wananchi.

Ametoa wito kwa maafisa habari kutumia kikao hicho kama fursa ya kufanya kazi kwa weledi na mshikamano ili kusaidia Serikali kuwasiliana vyema na wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here