Home UCHUMI Serikali Yaahidi kuimarisha uendelevu wa viwanda na biashara nchini

Serikali Yaahidi kuimarisha uendelevu wa viwanda na biashara nchini

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

SERIKALI imesema imejipanga kikamilifu kuimarisha uendelevu wa viwanda na biashara nchini kwa kuweka sera, sheria na mifumo rafiki itakayochochea ukuaji wa uchumi shindani na jumuishi.

Akizungumza leo Disemba,18 2025 na Waandishi wa Habari Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha sekta ya viwanda na biashara inakuwa mhimili mkuu wa mabadiliko ya kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji, ajira na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameeeleza kuwa wizara yake ina majukumu ya msingi ya kuandaa na kusimamia maendeleo ya viwanda na biashara, ikiwemo viwanda vidogo na kati, miundombinu ya viwanda, miliki bunifu, ushindani wa haki, viwango na ubora wa bidhaa pamoja na kukuza masoko na mauzo ya nje.

“Wizara inasimamia taasisi 13 ikiwemo TBS, NDC, SIDO, TIRDO, TEMDO, Wakala wa Vipimo, BRELA, TANTRADE, FCC, Bodi ya Stakabadhi za Ghala pamoja na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), zote zikiwa na lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kukuza viwanda,”amesema.

Amesisitiza kuwa sekta ya viwanda na biashara ni sekta wezeshi na ya uratibu, hivyo hufanya kazi kwa karibu na wizara na sekta nyingine ili kufanikisha malengo ya kitaifa ya maendeleo ya uchumi.

Akizungumzia Kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Kapinga amesema dira hiyo imeipa sekta ya viwanda na biashara kipaumbele kikubwa kwa kutambua uzalishaji wa viwandani kama msingi wa kuongeza mnyororo wa thamani, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira.

Ameongeza kuwa dira hiyo pia inasisitiza ushiriki mpana wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, akitaja ongezeko la thamani ya mauzo ya nje ya bidhaa na huduma hadi kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 14.7 katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa upande wa sekta binafsi, Kapinga amesema dira inaitambua kama injini kuu ya ukuaji wa uchumi huku serikali ikibaki kuwa mwezeshaji kupitia sera bora, sheria rafiki na miundombinu imara, kwa kuzingatia ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Kapinga amesema katika kipindi cha kwanza cha serikali ya awamu ya sita, wizara imefanya maboresho makubwa ya sera ikiwemo Sera ya Taifa ya Biashara, Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Sera ya Uendelezaji wa MSMEs ili ziendane na mazingira ya sasa ya kiuchumi na ushindani wa kimataifa.

Amesema maboresho ya sera yameanza kuleta matokeo chanya, ikiwemo ongezeko la mauzo ya nje ya bidhaa na huduma hadi kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 16.8, sambamba na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za viwandani na kilimo zilizoongezewa thamani.

Ametaja baadhi ya bidhaa zinazozalishwa kwa ziada kama saruji, mabati, vioo na bidhaa nyingine za viwandani ambazo sasa zinapelekwa katika masoko ya nje kutokana na uzalishaji mkubwa kuliko mahitaji ya ndani.

Amesema serikali pia imehuisha sheria zaidi ya 13 na kanuni mbalimbali zilizorahisisha taratibu za kuanzisha biashara, kupunguza gharama na muda wa kupata leseni, kuimarisha udhibiti wa vipimo na kuboresha mazingira ya uwekezaji.

“Kwa mujibu wake, maboresho haya yamesababisha ongezeko kubwa la usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara na leseni za viwanda, hali inayoashiria kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini,”amesema.

Kapinga ameongeza kuwa idadi ya viwanda imeongezeka kwa kasi, akitoa mfano wa Mkoa wa Pwani pekee ambapo zaidi ya viwanda 2,000 vimeanzishwa ndani ya miaka minne, vikiwemo zaidi ya 900 vya viwanda vidogo.

Amesema katika mwaka 2024 sekta ya viwanda ilichangia zaidi ya asilimia 7.3 ya Pato la Taifa huku sekta ya biashara ikichangia asilimia 8.6, ongezeko linalotokana na maboresho ya mazingira ya biashara na upanuzi wa masoko ya kikanda na kimataifa.

Kuhusu masoko ya nje, Kapinga amesema Tanzania imeendelea kunufaika na soko huru la biashara barani Afrika, Umoja wa Ulaya na Asia, ambapo mauzo ya bidhaa yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na mazao ya kilimo, bidhaa za viwandani na madini.

Amesisitiza kuwa serikali iko katika hatua za mwisho za kuandaa mkakati wa kitaifa wa mauzo ya nje ambao utawaweka vijana mbele katika kunufaika na fursa za masoko ya kimataifa, sambamba na kuendelea kuboresha mifumo ya kidijitali ya usajili na utoaji wa leseni kupitia BRELA.

Kapinga alihitimisha kwa kusema kuwa juhudi hizo zote zinalenga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi, unaotegemea viwanda vyenye tija, biashara yenye ushindani na sekta binafsi yenye nguvu kwa maendeleo ya Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here