Home MAKALA NDC yatakiwa kuweka kasi kufufua viwanda

NDC yatakiwa kuweka kasi kufufua viwanda

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi amelitaka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kutekeleza majukumu yake kwa uwajibikaji mkubwa ili kufanikisha malengo ya kitaifa.

Ameyasema hayo Disemba 18, 2025, wakati wa ziara yake katika shirika hilo ambapo amesema Serikali inalenga kufanya mapinduzi makubwa ya viwanda, kuanzia viwanda vidogo, vya kati hadi vikubwa, ili kuongeza nguvu za kiuchumi na nafasi za ajira nchini.

Aidha,amesisitiza kuwa maeneo yote yanayolengwa na taasisi lazima yasimamiwe kwa uaminifu, akimnukuu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhimiza uwekezaji mkubwa kwenye viwanda, utoaji wa mikopo na ushauri wa kibiashara ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

Amesisitiza pia umuhimu wa kushirikiana, kushauriana na kuondoa ukiritimba katika utekelezaji wa majukumu ya shirika na kuongeza kuwa NDC inapaswa kuwa daraja kwa wananchi na Serikali, sio kizuizi.

Katambi amesisitiza kuwa nchi zilizo na nguvu za kiuchumi ni zile zenye viwanda imara, jambo linaloipa nchi nafasi ya kutoa ajira kwa wananchi wake.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Valentine Simkoko, amesema shirika limeendelea kutekeleza majukumu yake pamoja na kusimamia mradi wa kimkakati wa uendelezaji wa viwanda nchini.

Ametaja mafanikio kuwa ni pamoja na uwekezaji katika miradi ya Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda Engareka, tathmini ya mali za wananchi wanaohusika na miradi ya makaa ya mawe Katewaka na Chuma Ghafi Maganga Matitu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here