Home KITAIFA Mambo: Amani,umoja na utulivu wa kisiasa ni msingi wa maendeleo ...

Mambo: Amani,umoja na utulivu wa kisiasa ni msingi wa maendeleo ya Taifa

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

KIJANA wa Kitanzania Masoud Mambo,  amesema amani, umoja na utulivu wa kisiasa ni nguzo muhimu za maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa bila amani hakuna haki, bila utulivu hakuna maendeleo, na bila umoja wa kitaifa hakuna Tanzania imara.

Akizungumza leo Disemba, 23 2025 jijini Dar es Salaam na  Waandishi wa Habari Mambo amesema wanaofanya vitendo hivyo ni wapinga maslahi ya Taifa na ustawi wa wananchi, hivyo hawapaswi kuungwa mkono kwa namna yoyote.

Amesema Watanzania wametakiwa kuwakataa na kuwapingana waziwazi watu au makundi yanayohamasisha au kuunga mkono mikakati inayolenga kuingiza nchi kwenye machafuko, vurugu au migawanyiko ya kisiasa.

“Watanzania tukumbuke tukiruhusu siasa za kuvuruga amani zitawale, waathirika wa kwanza tutakuwa ni sisi wenyewe sio hao walio ughaibuni au wanasiasa wenye viza tayari kukimbilia ughaibuni. Maendeleo yatasimama, uchumi utadorora na ajira zitapotea hivyo gharama ya kuyajenga upya itabebwa na sisi wananchi wenyewe,”amesema. 

Amesema Tanzania ni nchi inayotawaliwa na sheria Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vyote vilivyosajiliwa kisheria ni sawa mbele ya sheria bila ubaguzi wowote.

Ameongeza kuwa Demokrasia ya kweli haijengwi kwa mashinikizo, vitisho au siasa za misimamo mikali, bali hujengwa kwa hoja, ushindani wa sera na heshima kwa katiba na sheria za nchi. 

“Kila chama cha siasa kina haki ya kushiriki au kutoshiriki katika mchakato wowote wa kisiasa, lakini haki hiyo haiwezi na haitakiwi kutumika kama chombo cha kulazimisha nchi kuyumba au kuvuruga utulivu wa Taifa,”amesema.

Mambo amesema Tanzania imekuwa kimbilio la watu waliokimbia machafuko ya kisiasa katika mataifa yao hivyo wasikubali historia hii tukufu ibatilishwe kwa matakwa ya kisiasa ya muda mfupi.

Aidha ametoa wito kwa Watanzania wote kuiunga mkono serikali iliyopo madarakani katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa maslahi ya Taifa. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here