Home KITAIFA Mradi wa EACOP wafungua fursa za ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi

Mradi wa EACOP wafungua fursa za ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi

📌Ndejembi asema Watanzania 8,500 wamenufaika na Ajira za Moja kwa Moja

📌EACOP yakuza biashara za ndani na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kati ya Tanzania na Uganda.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaa

WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania (EACOP) umefungua fursa mbalimbali za ajira, biashara na maendeleo ya uchumi kwa Watanzania, hususani wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na mradi huo.

Akizungumza Januari 05, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kifupi na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Jamhuri ya Uganda, Dk. Ruth Nankabirwa, Mhe. Ndejembi amesema kuwa mradi huo umewezesha maelfu ya wananchi kupata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, sambamba na kunufaika na fursa za huduma na biashara wakati wa utekelezaji wake.

“Mradi wa EACOP umeleta manufaa makubwa kwa wananchi wetu kwa kutoa ajira takribani 12,000 za moja kwa moja, ambapo Uganda imenufaika na ajira 3,500 na Tanzania 8,500.

Aidha, mradi huu umechochea biashara za ndani na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi wa Taifa, hususan katika Jiji la Tanga, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kati ya Tanzania na Uganda,” amesema Ndejembi.

Amefafanua kuwa Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi na uendeshaji wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka maeneo ya Tilenga na Kingfisher nchini Uganda hadi kituo cha baharini kilichopo Chongoleani karibu na Bandari ya Tanga, Bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha mapipa 246,000 ya mafuta kwa siku.

Mradi huo unatekelezwa kupitia Kampuni ya EACOP Co. Ltd inayomilikiwa kwa pamoja na TotalEnergies, TPDC, UNOC na CNOOC, na ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, Mradi wa EACOP unajumuisha ujenzi wa Kituo cha Kuhifadhi na Kusafirisha Mafuta cha Baharini (Marine Export Terminal) kilichopo Chongoleani, chenye matangi manne makubwa ya kuhifadhi mafuta pamoja na gati la baharini lenye urefu wa kilomita 2.

Ndejembi amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 79 na shughuli za ujenzi zipo katika hatua za juu. Inatarajiwa kuwa mradi utakamilika Julai 2026 huku shehena ya kwanza ya mafuta ikitarajiwa kusafirishwa kupitia Bandari ya Tanga mwezi Oktoba 2026.

Amesema umeme wa kuendesha mradi huo utatoka kwenye gridi za Taifa za Uganda na Tanzania ukisaidiwa na umeme wa akiba pamoja na nishati ya jua yenye uwezo wa megawati 4 hatua inayolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inathamini ushirikiano wa karibu na Serikali ya Uganda pamoja na kampuni za kimataifa za TotalEnergies na CNOOC katika utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati kwa maendeleo ya Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dk. Ruth Nankabirwa, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira ya dhati katika kuhakikisha mradi wa EACOP unatekelezwa kwa mafanikio makubwa.

Amesema kuwa awali walikuwa wakifuatilia maendeleo ya mradi kupitia mawasilisho ya kitaalamu, hivyo kuona umuhimu wa kufika nchini Tanzania kujionea hali halisi ya utekelezaji wake. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na utaratibu maalum wa kuwatambua watumishi wanaopata ajira katika miradi ya kimkakati ili waweze kupewa kipaumbele katika miradi mingine ijayo, ikiwemo miradi ya gesi na umeme inayotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizo.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga, una urefu wa kilomita 1,443 ambapo kilomita 296 zipo Uganda na kilomita 1,147 zipo Tanzania Kwa upande wa Tanzania, mradi una vituo vinne vya kusukuma mafuta, huku Uganda ikiwa na vituo viwili na kufanya jumla ya vituo vya kusukuma mafuta kuwa sita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here