Home AFYA Mtoto aliyesaidiwa na Dk. Samia aanza matibabu ya kibingwa MOI

Mtoto aliyesaidiwa na Dk. Samia aanza matibabu ya kibingwa MOI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MTOTO Nicholaus Nkinga (9) ambaye changamoto yake ya matibabu ya mguu iliyomgusa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameanza rasmi kupata matibabu ya kibingwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Jijini Dar es Salaam.

Mtoto huyo mwenye changamoto ya kuvunjika mguu wa kushoto alipokuwa akicheza mpira Mwaka Mmoja na Miezi Sita iliyopita katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, amepokelewa leo Januari 5, 2026 katika taasisi ya MOI na kuanza matibabu akiwa ameambatana na mama yake mzazi.

Mama wa mtoto huyo Lucia Kawawa ameipongeza Taasisi ya MOI kwa mapokezi mazuri huku akimshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa wa upendo na huruma na kugharamia matibabu ya mwanae.

“Ninamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa upendo na huruma… Mtoto wangu sasa ameanza matibabu jambo amabalo sikuwa na uwezo wa kulitelekeza peke yangu” amesema Lucia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya amesema taasisi hiyo imempokea mtoto huyo na tayari madaktari bingwa bobezi wameanza taratibu zote za uchunguzi na matibabu kulingana na hali yake.

“Tumempokea mtoto Nicholous na ameanza matibabu, tunamshukuru Mhe: Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuibua mtoto huyu na kumleta hapa MOI, madaktari bingwa wanaendelea na matibabu…najua watu wenye changamoto za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu wapo wengi kwenye jamii yetu” amesema Dk. Mpoki na kuongeza kuwa

“Wale wenye changamoto hizo wanaweza kuwasiliana nasi kwa namba ya simu 0733803104, ukipiga namba hii itapokelewa na mtoa huduma kwa wateja ambaye utamweleza tatizo lako na kisha taasisi itaangalia namna ya kukusaidida”

Amesema kuwa katika jitihada za taasisi kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi amesema hivi karibuni madaktari bingwa bobezi wataweka kambi maalum ya matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara.

“Natoa wito kwa wananchi wenye changamoto za mifupa, ubongo mgongo na mishipa ya fahamu kujitokeza kwa ajili ya kupatiwa matibu wakati wa kambi hiyo,” amesema Dk. Mpoki.

Naye, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga Bi. Swaiba Chemchem amemshukuru Rais Samia kwa moyo wa upendo na huruma kwa wenye uhitaji na kufanikisha safari ya matibabu ya mtoto huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here