Home KITAIFA Rais Dk. Mwinyi afungua flyover Zanzibar

Rais Dk. Mwinyi afungua flyover Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itawalipa fidia wananchi wote waliopisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao, akisisitiza kuwa hakuna mwananchi atakayodhulumiwa haki yake.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari, 6 2025 wakati wa hafla ya ufunguzi wa Barabara ya Juu (Flyover) ya Dk. Hussein Ali Mwinyi – Mwanakwerekwe, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa Serikali tayari imeunda Kamati Maalum ya uhakiki na tathmini ya fidia katika maeneo yaliyopitiwa na miradi ya maendeleo, kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi analipwa stahiki yake kwa haki na kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanachochewa na uwepo wa miundombinu bora, hususan barabara, na amewataka wananchi kuwa tayari kushirikiana na Serikali kwa kupisha miradi ya maendeleo kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla.

“Ujenzi wa barabara, madaraja na flyover unaongeza thamani ya ardhi na nyumba, hivyo ni muhimu wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao,” amefafanua.

Aidha, amesema kuwa ujenzi wa Flyover hiyo ni wa kihistoria na ni ushahidi wa dhana ya uongozi unaoacha alama, akiwataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo na kuacha kujenga katika maeneo ya hifadhi ya barabara, ambayo yametengwa mahsusi kwa ajili ya miundombinu ya maji, umeme na mawasiliano.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Bandari ya Mpiga Duri – Shumba, na hivi karibuni kuanza kwa ujenzi wa Bandari ya Wete, hatua inayolenga kuifungua Zanzibar kiuchumi na kuharakisha maendeleo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhammed, amepongeza jitihada na mafanikio ya Rais Dk. Mwinyi katika kipindi cha uongozi wake, hususan mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya miundombinu ya barabara ambayo yameleta maboresho makubwa katika usafiri.

Akitoa taarifa ya kitaalamu ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Ali Said Bakari, amesema ujenzi wa Flyover ya Dk. Hussein Ali Mwinyi uliotekelezwa na Kampuni ya CCECC umegharimu jumla ya shilingi bilioni 23.7.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here