Home UCHUMI BoT yazidi kudumisha Riba ya asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza...

BoT yazidi kudumisha Riba ya asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026

Na Esther Mnyika,Dar es Salaam

KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kwamba riba kuu ya benki (CBR) itabaki kuwa asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026 kutokana na matarajio chanya ya ukuaji wa uchumi na mwenendo thabiti wa mfumuko wa bei nchini.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya tathmini ya hali ya uchumi wa ndani na wa kimataifa, huku kamati ikizingatia kuwa mfumuko wa bei umekuwepo katika kiwango cha kuridhisha, na kutarajia kuendelea kudumisha hali hiyo.

Riba hiyo imetangazwa leo Januari, 8 2025 jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema wataendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia, ambapo mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini ya lengo la asilimia tano na hali hiyo itasaidia kukuza shughuli za kiuchumi.

Ameongeza kuwa, hali hiyo inawawezesha kuwa na mazingira ya kuchochea ukuaji wa uchumi, huku viwango vya riba vikibaki vya wastani, hivyo kusaidia sekta mbalimbali kuendelea kukua.

“Uamuzi wa kubakiza CBR unakuja wakati ambapo uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.2 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 3.3 mwaka 2024. Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kuwa, kwa vile bei ya mafuta ghafi inashuka, uchumi wa dunia utaendelea kuwa msaada mkubwa katika kudumisha mfumuko wa bei chini ya lengo la asilimia tano jambo ambalo linachochea utulivu wa kiuchumi ndani ya nchi,”amesema.

Kwa upande mwingine, bei ya dhahabu imeendelea kupanda na kufikia kiwango cha juu cha dola za Marekani 4,421.65, hali ambayo inatarajiwa kuimarisha mapato ya fedha za kigeni na kupunguza shinikizo la viwango vya mfumuko wa bei.

Amesema hiyo inatoa matumaini kwamba uchumi wa Tanzania utaendelea kupanuka na kuwa na misingi imara ya kuhimili changamoto za kimaisha.

UKUAJI WA UCHUMI WA NDANI NA MATOKEO YA SERA YA REDHA

Tathmini ya uchumi wa ndani inaonesha kwamba uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025, huku Zanzibar ikiwa na ongezeko la asilimia 6.8.

Uchumi wa Zanzibar unachangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, utalii, na uzalishaji viwandani, huku Tanzania Bara ikiongozwa na sekta za kilimo, madini na ujenzi.

Kamati pia imetathmini sekta ya benki, ambapo imebainika kuwa benki nchini zinaendelea kuwa na ukwasi wa kutosha kutoa mikopo, huku viwango vya mikopo chechefu vikishuka hadi kufikia asilimia 3.1, chini ya ukomo wa asilimia tano na hiyo ni ishara ya imani ya wadau katika mfumo wa kifedha wa nchi, na inatoa matumaini kuwa benki zitaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

HALI YA FEDHA ZA KIGENI NA UCHUMI WA KIMATAIFA

Gavana Tutuba amesema sekta ya nje inatarajiwa kuimarika, hasa kutokana na ongezeko la mauzo ya madini, hususan dhahabu, na mazao ya kilimo.

“Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida inakadiriwa kupungua hadi asilimia 2.2 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2025, ikiwa ni kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hali hii inatoa mwelekeo mzuri kwa sekta ya fedha za kigeni, huku akiba ya fedha za kigeni ikiwa juu ya lengo la miezi minne na inatarajiwa kuwa na utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine.

Matumaini ya Robo ya Kwanza ya mwaka 2026 kwa kuzingatia hali hii ya uchumi wa dunia na wa ndani, Kamati ya Sera ya Fedha imeonyesha matumaini ya kuwa riba kuu ya Benki Kuu (CBR) itasaidia katika kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha mazingira mazuri kwa sekta binafsi na za serikali, “amesema.

Amesema kamati inatarajia kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, uchumi wa Tanzania Bara utaendelea kukua kwa asilimia sita huku Zanzibar ikitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2.

“Tathmini ya uhimilivu wa deni la serikali inaonesha kuwa uwiano wa deni la umma kwa Pato la Taifa umeendelea kuwa chini ya ukomo unaokubalika kimataifa. Uwiano huu ulipungua hadi asilimia 40.6 kwa mwaka 2024/2025, kutoka asilimia 41.1 mwaka 2023/2024,hii inaonesha kuwa serikali inaendelea kusimamia vyema deni la taifa, huku ikikusanya mapato ya kutosha,”amesema.

MATARAJIO MWAKA HUU

Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kuwa sera hiyo itasaidia kuendelea kudumisha mfumuko wa bei katika kiwango cha asilimia tatu hadi tano na kutoa nafasi kwa uchumi wa Tanzania kuendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha.

Amesema uamuzi huo utazidi kuchochea shughuli za kiuchumi nchini na kusaidia kuimarisha utulivu wa fedha za kigeni.

“Kamati inatarajia kukutana tena Aprili 2, 2026, kwa kikao kingine cha kujadili hali ya uchumi na kuamua kiwango cha riba kuu kwa robo ya pili ya mwaka 2026.

MWAKILISHI WA MABENKI NCHINI

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Umoja wa mabenki Nchini, Herman Kasekende ametoa shukrani za dhati kwa Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa sera ya kifedha, akisema kuwa hatua hizo zimechangia kuimarika kwa sekta ya kilimo na ukuaji wa uchumi.

Amekubaliana na juhudi zinazofanywa katika kuhakikisha kuwa ongezeko la bei halijathiri ukuaji wa GDP, huku akisisitiza umuhimu wa kushukuru kwa kudumisha hali ya utulivu katika sekta ya mafuta, licha ya changamoto zilizopo duniani.

Ameeeleza kuwa kuridhishwa na kupungua kwa upungufu wa bajeti kutoka asilimia tano hadi asilimia 2.2, akielezea kuwa ni mafanikio makubwa.

Ameongeza kuwa, licha ya changamoto nyingi zinazojitokeza, mabenki yameendelea kutoa huduma kwa sekta binafsi kwa msaada wa BoT.

Vilevile, amegusia masuala ya ufanisi katika usimamizi wa sarafu na changamoto zinazohusiana na mikopo ya binafsi, akitaka ushirikiano zaidi kati ya Benki Kuu, Wizara ya Fedha na Mabenki ili kumaliza masuala ya uandishi wa mikopo na sheria za kodi zinazohusiana na hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here