Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Nondo amesema kuwa sera ya maendeleo endelevu ya viwanda ya mwaka 2023, pamoja na Dira ya Taifa 2025 na 2050, inalenga kuimarisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuchochea uchumi wa ndani.

Hayo amebainisha leo Januari,23 2026 Jijini Dar es Salama wakati alipotembelea Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) Nondo amesema wizara inaendelea kusimama pamoja na taasisi zinazotekeleza ajenda ya maendeleo ya viwanda nchini.
Amesena kuwa viwanda ndiyo nguzo kuu ya ukombozi wa kiuchumi wa Taifa na chachu ya ajira, ubunifu na ustawi wa vijana, akisisitiza kuwa Tanzania haiwezi kukwepa kuwekeza kikamilifu kwenye sekta ya viwanda kama inataka kufikia maendeleo ya kweli.
“Msingi wa kuanzishwa kwa shirika la maendeleo ya viwanda mwaka 1979 ulikuwa ni kulinda na kukuza hatima ya sekta ya viwanda katika nchi changa, akisema kuwa leo, zaidi ya miongo minne baadaye, umuhimu wa taasisi hiyo umeongezeka maradufu kutokana na changamoto za uchumi wa dunia na ushindani wa kiteknolojia,”amesema.

Nondo ameeleza kuwa viwanda vinaongoza katika uundaji wa ajira na kuimarisha usalama wa kiuchumi wa nchi, huku pia vikiwa chanzo kikuu cha ubunifu na matumizi ya teknolojia miongoni mwa vijana, ambao sasa wanahitaji mazingira rafiki ya kuendeleza mawazo yao ya kibiashara.
Pia ameipongeza taasisi hiyo kwa kuwakuza wajasiriamali kutoka mitaani na kuwageuza kuwa wazalishaji wakubwa, akitaja mfano wa kijana aliyebuni mtambo wa kuchakata taka za plastiki na kuzalisha nishati, hatua ambayo inalinda mazingira na kuongeza ajira.

Aidha ameahidi kuchukua hoja za wadau na kuzifikisha katika ngazi ya wizara ili kuweka mifumo bora ya kuwawezesha wajasiriamali katika halmashauri zote nchini, akisisitiza ushirikiano kati ya taasisi za serikali, sekta binafsi na mamlaka za mitaa.
Ametoa wito kwa Watanzania kuweka maslahi ya Taifa mbele, kufanya kazi kwa mshikamano na kujifunza kutokana na mafanikio na makosa ya wengine. “Viwanda ni moyo wa uchumi; tukiviimarisha, tutaipa Taifa damu ya maendeleo.”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Mtambo amesema wanataraji kuanzisha kituo cha kutengeneza na matengenezo ya vifaa vya umeme kwaajili ya kukuza ubunifu wa ndani kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje.



