Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mabadiliko ya tabia nchi si nadharia bali ni uhalisia unaoendelea kuathiri maisha ya watu duniani kote.

Akizungumza na wananchi katika eneo la Bungi Kilimo leo Januari 27, 2025 Mkoa wa Kusini Unguja, Rais Samia amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaonekana wazi kupitia kuongezeka kwa ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko makubwa, ongezeko la joto pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari.
“Mabadiliko ya tabia nchi si hadithi, ni uhalisia tunaouona na kuishi nao. Nchi zote duniani zinakabiliwa na athari hizi,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa upandaji wa miti ni mojawapo ya njia mahsusi na endelevu za kukabiliana na changamoto hizo, akisisitiza kuwa mti unaopandwa na kutunzwa leo una mchango mkubwa katika kuleta mvua, kuhifadhi vyanzo vya maji, kulinda ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na kuimarisha ustawi wa wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

Aidha, amesema suala la uhifadhi wa mazingira ni miongoni mwa nguzo muhimu za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika eneo la uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi.

Ameongeza kuwa kwa makisio ya idadi ya watu kufikia milioni 70 katika miaka ijayo, endapo Watanzania milioni 30 watapanda mti mmoja kila mwaka na kuutunza hadi ukue, taifa litakuwa na ongezeko kubwa la miti na mazingira endelevu.



