Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
NDANI ya siku 100 tangu aanze utekelezaji wa ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameweka msingi imara wa mageuzi ya elimu kwa kuzindua Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali, darasa la kwanza na la pili.

Akizungumza Leo Januari, 29 2026 jijini Dar es Salaam jana katika hafla yauzinduzi wa mpango huo, Rais Dk. Samia amesema serikali imeamua kushughulikia changamoto za elimu kuanzia kwenye mizizi yake, badala ya kusubiri matatizo yajitokeze katika ngazi za juu za elimu.
Amesema uzinduzi wa mpango huo unaonesha dhamira ya dhati ya serikali ya kuboresha matokeo ya ujifunzaji kwa watoto hivyo stadi za KKK ndizo msingi wa elimu yote na maendeleo ya taifa.
“Mpango huy una kauli mbiu ya KKK ni Msingi wa Elimu kwa Maendeleo Endelevu na kwamba umebuniwa kuwajengea watoto uwezo wa kukabiliana na masomo yao katika mazingira yanayobadilika duniani, huku ukichangia pia katika ujenzi wa uchumi wa taifa,”amesema.
Amesema bila msingi huo, jitihada nyingine zote za maendeleo zitakuwa hazina tija ya kudumu.
Ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza maendeleo ya rasilimali watu na taifa linaloongozwa na maarifa na uadilifu hivyo mpango huo unatekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo inayolenga kumwezesha mwananchi kuchangia maendeleo ya taifa.

Amesema serikali inaweza kujenga miundombinu bora ya elimu na kukuza teknolojia, lakini bila kuimarisha msingi wa elimu ya awali, taifa litakuwa linajenga juu ya msingi dhaifu ambapo hapo nyuma, udhaifu wa msingi huo uliathiri matokeo ya wanafunzi walipohitimu elimu ya msingi.
Rais Dk.Samia amesema serikali imefanya maboresho ya mitaala ya elimu ya lazima kuwa ya miaka 10 ili kuhakikisha watoto wanapata maandalizi thabiti na sawa kabla ya kuendelea na ngazi nyingine za elimu.
“Mkakati wa KKK ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya kikanda na kimataifa, ikiwemo Azimio la Umoja wa Afrika kuhusu elimu ya Afrika katika karne ya 21 na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, hususan lengo namba nne,”amesema.
Akizungumzia teknolojia, Rais Dk.Samia alisema watoto wa kizazi cha sasa wanapaswa kuendana na mabadiliko hayo na kutokana na hilo alisema amevutiwa na maonyesho ya zana za kufundishia zilizobuniwa ndani ya nchi kwa kutumia vifaa rahisi lakini vyenye ufanisi mkubwa.
Ameeleza kuwa maonyesho hayo yameonesha kuwa watoto wanaweza kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu kupitia vitendo, michezo na ushiriki wa moja kwa moja badala ya nadharia pekee.
Rais Dk.Samia ameipongeza wizara kwa kuzingatia ujumuishi hususani kwa watoto wenye mahitaji maalum wakiwa wamezingatiwa katika mpango huo, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma.
Amesisitiza kuwa katika dunia ya sasa, kuwekeza katika stadi za awali za elimu si hiari bali ni wajibu wa serikali, wazazi na jamii kwa ujumla hivyo aliwataka watmdau wote wa elimu kutoa ushirikiano.

Rais Dk. Samia amesema serikali imeongeza juhudi katika uandikishaji wa wanafunzi na ujenzi wa miundombinu ya elimu, ambapo idadi ya madarasa ya shule za msingi na sekondari imeongezeka kwa kiwango kikubwa kati ya mwaka 2021 na 2025.
“Serikali imefanya jitihada kubwa katika kuboresha upatikanaji elimu kwa kuongeza kiwango cha uandikishaji na kuimarisha miundombinu katika shule za msingi na sekondari.
Katika elimu msingi madarasa yameongezeka kutoka 151, 315 mwaka 2020 / 2021 hadi madarasa 184, 550 mwaka 2020/2025 na upande wa elimu ya sekondari madarasa hayo yameongezeka kutoka 64, 204 mwaka 2021 hadi 101473 , mwaka 2025 na takwimu hii inatuonesha tumetoka mbali,” amesema.
Amesema kwa upande wa sekondari kwa kipindi cha miaka minne kutoka mwaka 2021 hadi 2025 wamejemga madarasa 9317 kila mwaka , hatua zote hizo ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma, kwanza ni kuwavuta na kuwaleta ndani ya darasa, na darasa liwe rafiki kumfanya mtoto aweze kusoma na kuelewa vizuri.
Katika kipindi hicho Serikali imeongeza kasi ya ujenzi wa madarasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo kwa wastani wa miaka 60, Tanzania ilikuwa ikijenga madarasa 3,080 ya msingi kwa mwaka, ikilinganishwa na wastani wa zaidi ya madarasa 8,000 kwa mwaka katika kipindi cha sasa.
Amesema sekta binafsi nayo imekuwa ikifanya kazi kubwa katika utoaji wa elimu nchini kuanzia awali hadi ngazi ya juu hivyo serikali inathamini nguvu au mchango wao.
” Katika suala la watumishi wa elimu katika ahadi zangu za siku 100 tuliahidi tutaajiri walimu 7000 ninayo furaha kusema tumeshaajiri na kuwapangia vituo vya kazi walimu 644 na walinu 956 wapo kwenye mchakato kujaza nafasi zilizobaki ili tutakapofika Februari 3, tuwe tumemaliza nafasi zote 7000,” amesema.
Amesema maboresho pekee hayatoshelezi ikiwa hatutasimamia ipasavyo ubora wa mafunzo.
Amesisitiza kuwa ujenzi wa miundombinu na ajira za walimu havitoshi bila kusimamia ubora wa mafunzo yanayotolewa, hususan katika hatua za mwanzo za ukuaji wa mtoto.
“Serikali imejipanga kuhakikisha waliju wanakuwa sehemu ya suluhusho na wadau muhimu katika utekelezaji wa makakatu huu kwa kuwapatia nyenzo , mafunzo na mbinu za kisasa katika ufundishaji,”amesema.
Rais Dk.Samia amewataka wakaguzi wa elimu kuhakikisha mpango wa KKK unasimamiwa kikamilifu katika shule zote na kusisistiza kuwa matokeo ya mpango huo lazima yaonekane moja kwa moja kwa mtoto darasani.

Aliitaka Wizara ya Elimu, TAMISEMI na wizara husika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu na hauishii kwenye makaratasi bali unaleta matokeo yanayopimika.
Amewataka wazazi na jamii, kushirikiana na serikali katika kufanikisha mpango huo kwa sababu elimu ya awali huanzia nyumbani kabla ya kuendelea shuleni.
Nayec Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alimpongezwa Rais Dk.Samia kwa kutimiza ahadi yake kwa Watanzania ya kuandaa na kuzindua mpango mkakati wa kisayansi wa kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ndani ya siku 100 tangu kuunda serikali yake.
Alisema mpango huo umeandaliwa kwa kina na umezingatia maeneo makuu matano muhimu ikiwemo kuimarisha ufundishaji kwa kutoa mafunzo endelevu kwa walimu, hususan walimu wa elimu ya awali, darasa la kwanza na la pil ili kuboresha mbinu bora za ufundishaji.
Aidha, mpango unalenga maendeleo endelevu ya walimu kwa kuwashirikisha kikamilifu katika maandalizi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Eneo lingine muhimu ni upatikanaji wa nyenzo za kufundishia na kujifunzia zinazotokana na mazingira halisi ya Tanzania, ikiwemo matumizi ya vifaa rahisi kama vizibo vya chupa za soda.
Amesema vifaa hivyo ni sehemu ya sayansi ya mpango huo, unaoeleza umuhimu wa kuwajengea watoto umahiri wa stadi hizo ndani ya miaka minane ya awali ya makuzi yao na umeweka mkazo kwenye tathmini na upimaji wa mara kwa mara kuhakikisha maendeleo yanapimwa na kufuatiliwa ipasavyo.
Profesa Mkenda ametaja eneo lingine ni ushirikishwaji wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla katika kukuza elimu ya watoto hivyo alisisitizauwa baada ya uzinduzi huo, kutakuwa na ufuatiliaji wa karibu kwa kushirikiana na TAMISEMI ili kuhakikisha utekelezaji wake unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema baraza hilo limekuwa likiendesha upimaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa njia ya sampuli tangu mwaka 2015, kwa lengo la kufuatilia kwa karibu kiwango cha umahiri wa wanafunzi katika hatua za awali za elimu.
“Upimaji huu ulihusisha wanafunzi wa darasa la pili kutoka shule chache zilizochaguliwa katika kila halmashauri nchini na ukusanyaji wa taarifa muhimu kutoka kwa walimu wakuu kuhusu mazingira ya ujifunzaji, ufundishaji, upatikanaji wa vitabu na uwepo wa walimu waliopata mafunzo,” amesema.
Ameeleza kuwa matokeo ya upimaji huo kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2023 yalibainisha kuwa wanafunzi wengi walikuwa na umahiri mdogo katika stadi za KKK, huku umahiri mzuri zaidi ukionekana katika stadi za kusoma na kuandika.
Amefafanua kuwa wanafunzi wengi waliweza kusoma kwa ufasaha maneno rahisi yenye silabi moja au zenye konsonanti na irabu, lakini walipata changamoto kusoma maneno yenye silabi changamani, vinyongo na maneno yanayohitaji kasi na ufasaha zaidi.
Kwa upande wa stadi za kuhesabu, Profesa Mohamed amesema changamoto kubwa zilizobainika ni pamoja na kushindwa kubaini namba zinazokosekana, kufanya hesabu za kujumlisha kwa kubeba, kutoa kwa kukopa, pamoja na kutafsiri maneno yanayoelezea matendo ya kihisabati kama vile kupungua, kuongezeka na kubaki.
Amesema changamoto hizo ziliathiri uwezo wa wanafunzi kufumbua mafumbo ya kihisabati katika ngazi ya msingi.
Ameeleza kuwa kufuatia changamoto hizo, NECTA kwa kushirikiana na wadau wa elimu ilichukua hatua za makusudi ikiwemo kutoa mafunzo ya upimaji wa KKK kwa walimu wa elimu ya awali, walimu wa darasa la kwanza na la pili, wakuu wa shule, maafisa elimu taaluma pamoja na wadhibiti ubora katika mikoa na halmashauri zote nchini.
Mafunzo hayo yalihusisha walimu zaidi ya 43,000 na yalilenga kuimarisha ufundishaji na ufuatiliaji wa stadi za KKK mapema kabla ya mwanafunzi kufika ngazi za juu.
Profesa Mohamed ameongeza kuwa maboresho hayo yameanza kuzaa matunda, ambapo takwimu za upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kuanzia mwaka 2022 hadi 2025 zinaonyesha kupungua kwa idadi ya wanafunzi wasiomudu stadi za KKK mwaka hadi mwaka
Amesema hali hiyo ilithibitisha umuhimu wa kuanza kupima na kushughulikia changamoto za KKK mapema, badala ya kusubiri mwanafunzi afike darasa la nne, hatua ambayo mara nyingi huwa ni kuchelewa.
Amesisitiza kuwa jamii inapaswa kuacha dhihaka na mitazamo hasi dhidi ya somo la hesabu, akieleza kuwa dhihaka hizo hujenga hofu kwa wanafunzi na kuathiri moja kwa moja ujifunzaji wao.
Amesema dunia inaendeshwa na sayansi na hisabati, hivyo kuendelea kulidharau somo hilo ni kujinyima fursa ya maendeleo, akihimiza wadau wote wa elimu kulichukulia somo la hesabu kama msingi muhimu wa maendeleo ya elimu na taifa kwa ujumla.
Awali Mkuu wa Mkoa, wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema jambo hilo lina tija na linakwenda kuthibitisha kuwa Dar es Salaam kuwa mdau mkubwa katika utekelezaji wa programu hiyo.
Akizungumza kuelekea uzinduzi wa programu hiyo, alisema mkoa huo unajumla ya wanafunzi wa shule ya msingi 855,000 na sekondari 500,000.
Amesema mkoa huo una mchango mkubwa chini ya usimamizi wa Rais, hususan katika kuandikisha wanafunzi wa shule ya awali na darasa la kwanza, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali kuwekeza kwenye elimu ya msingi.
Amefafanua kuwa hadi sasa wanafunzi 32,000 wa shule ya awali tayari wameshasajiliwa, sawa na asilimia 24 ya lengo lililowekwa, huku matarajio yakiwa kufikia usajili wa wanafunzi 132,000.
Kwa upande wa darasa la kwanza, Dar es Salaam imeshapewa idadi ya wanafunzi 87000 wakati bajeti ya awali ilikuwa ni kuandikisha wanafunzi 95,000 jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wazazi na jamii kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya programu hiyo yanategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa watoto kuwa wamiliki na watendaji mahiri wa lugha inayotumika kufundishia.
Amesema bila watoto kuwa na umiliki na umahiri wa lugha hiyo, malengo ya elimu hayawezi kufikiwa ipasavyo.
Ameeleza kuwa kuimarisha stadi za lugha, hususan katika ngazi ya awali, kutarahisisha ujifunzaji wa masomo yote, kwani msingi wake ni uelewa wa maana au semantiki ya lugha, hatua itakayosaidia kujenga rasilimali watu yenye uwezo mkubwa kwa maendeleo ya taifa.



