Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wanafunzi wanaopata fursa ya kusoma nje ya nchi wanapaswa kuzingatia maadili, nidhamu na bidii katika masomo yao na kufanya hivyo kutawawezesha kurejea nchini wakiwa na maarifa na ujuzi utakaotoa mchango chanya katika maendeleo ya Taifa.

Pia amesema wameanza utekelezaji kwa vitendo wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia, baada ya kuwaaga wanafunzi 16 kati ya 50 waliopata ufadhili wa masomo ya juu nje ya nchi kupitia mpango wa ‘Samia Scholarship’
Akizungumza leo Januari 30, 2026 jijini Dar es Salaam Profesa Mkenda amesema ufadhili huo unalenga kuongeza idadi ya wataalamu katika maeneo ya sayansi ya data, akili unde na teknolojia ya viwanda.Pia wanafunzi hao wanaelekea katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa masomo yanayolenga kuzalisha wataalamu bingwa katika sayansi ya data, akili unde na teknolojia ya viwandani.
“Wanafunzi hawa wametoka katika shule mbalimbali zikiwemo shule za serikali na binfsi wanafunzi kati ya wanafunzi 50 waliochaguliwa, 16 wanaanza masomo Chuo Kikuu cha Johannesburg huku 34 wakitarajiwa kuendelea na masomo katika vyuo vikuu vya Ireland,”amesema.

Amesema serikali imeahidi kuwekeza kwenye sayansi kwa lengo la kuzalisha wataalamu katika teknolojia ya tehama, sayansi ya data, akili unde, sayansi ya kompyuta na teknolojia ya viwandani.
Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa Sayansi ya Nyuklia licha ya kuwa na madini ya urani, hali inayozuia nchi kunufaika kikamilifu na rasilimali hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi, Dk. Amos Nungu amesema ufadhili huo utachochea maendeleo ya sayansi na teknolojia hususani katika eneo la akili unde na kutoa mtazamo mpya wa maendeleo ya sayansi nchini.
Mmoja wa wanufaika wa ufadhili huo, Malaika Florence amesema wengi wao walikuwa hawana ujuzi w msingi wa matumizi ya kompyuta lakini sasa wamejifunza stadi za kisasa ikiwemo uandishi wa codes na matumizi ya lugha mbalimbali.

“Tumejengewa uwezo na misingi mbalimbali ikiwemo mafunzo ya kompyuta, usimamizi wa fedha na maarifa ya kuijua duniaTunalijua taifa limetuamini. Tunaahidi kusoma kwa bidii ili tuwe sehemu ya kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.



