Home KITAIFA Mavunde azindua urushwaji wa helikopta ya utafiti wa kina wa madini

Mavunde azindua urushwaji wa helikopta ya utafiti wa kina wa madini

▪️Ni utafiti utakaofanywa na Kampuni ya Barrick kwa ajili ya uanzishwaji wa mgodi mpya

▪️Utagusa maeneo ya Msalala, Nzega,Nyangh’wale, Igunga na Mbogwe

▪️Waziri Mavunde aelekeza wachimbaji wadogo kupewa maeneo ambayo hayatatumiwa kwa uwekezaji mkubwa

▪️Utafiti huu kuongeza eneo la Utafiti wa madini wa kina nchini

Na Mwandishi Wetu, Kahama

IKIWA ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuhakikisha inafikia lengo la kuongeza eneo la utafiti kufikia asilimia 50 ifikapo 2030, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amezindua urushwaji wa Helkopta iliyofungwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya utafiti wa madini nchini.

Amefanya uzinduzi huo leo Februari, 1 2026 katika eneo la Buzwagi Wilayani Kahama kuashiria kuanza rasmi utafiti utakaofanywa na Kampuni ya Barrick kwa ajili ya uanzishwaji wa mgodi mpya.

“Kupitia Dira ya Madini 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza kuhakikisha tunaongeza eneo la utafiti wa kina wa madini kupitia uwekezaji wa Serikali na Sekta binafsi, “amesema Mavunde.

“Tunachokifanya leo hapa ni kiashiria tosha kwamba maono hayo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan yanakwenda kufikiwa ipasavyo. Tunaishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuamua kuunga mkono juhudi hizi za Serikali kwa vitendo,” ameeleza.

Waziri Mavunde pia amebainisha kwamba utafiti huo unaofanywa na Barrick unahusisha helkopta kuruka katika maeneo ya Msalala, Nzega, Igunga, Mbogwe na Nyangh’wale kwa lengo la kupata taarifa zitakazosaidia uanzishwaji wa mgodi mpya.

Kwa maeneo ambayo Barrick itafanya utafiti na kuona hayakidhi vigezo vya uchimbaji mkubwa, Mhe. Mavunde alielekeza kuwa maeneo hayo yatagawiwa kwa wachimbaji wadogo ili kuwaongoza na kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.

Awali, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick Tanzania, Dk. Melkiory Ngido amebainisha kwamba tangu ianze shughuli zake nchini Tanzania mwaka 2020, Kampuni imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 100 kwenye utafiti wa kina wa madini, na kupitia migodi mitatu inayoiendesha imeweza kuleta nchini thamani ya zaidi ya trilioni 14 kwenye mzunguko wa uchumi wa ndani.

Akitoa Salaam za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ameishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini ambayo yamewezesha Kampuni ya Barrick kuendelea kufikiria kuongeza uwekezaji nchini.

Nao, wabunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa na wa Jimbo Msalala, Mabula Magangila wameishukuru Serikali kwa namna inavyowezesha uwekezaji Wilayani Kahama na kueleza matarajio ya wananchi kuwa watakwenda kupata ajira na kuwainua kiuchumi kupitia miradi itakayokwenda kuanzishwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here