Home KITAIFA Serikali yabainisha Maeneo ya Miradi ya Umeme wa Upepo na Jua, Kishapu...

Serikali yabainisha Maeneo ya Miradi ya Umeme wa Upepo na Jua, Kishapu kuzalisha MW 150

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema Serikali imekwishabainisha na kufanya utafiti wa maeneo mbalimbali yanayofaa kuendelezwa kwa ajili ya miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo na jua, ikiwa ni pamoja na Zuzu-Dodoma, Same-Kilimanjaro na Manyoni-Singida.

Ametoa kauli hiyo leo Februari 05, 2026 Salome Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwera, Suleiman Mohamed Rashid aliyehoji juu ya mpango wa Serikali wa kutumia vyanzo vya umeme na upepo juu vilivyopo nchini.

” Kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 150 katika Wilaya ya Kishapu, Shinyanga ambapo awamu ya kwanza ya mradi huo wenye megawati 50 imekamilika na hatua za kuingiza umeme huo katika Gridi ya Taifa zimeanza,” amesema Salome.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro, Esther Malleko aliyehoji mkakati wa Serikali katika kumaliza usambazaji wa umeme kwenye vitongoji vilivyosalia mkoani humo, Salome amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na kazi za utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo hadi kufikia Januari 2026 jumla ya vitongoji 2,032 kati ya 2,258 sawa na asilimia 90 vilipatiwa umeme na kusalia vitongoji 226 ambavyo vitapelekewa umeme kupitia miradi mbalimbali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here