Home KITAIFA Chalamila aagiza ujenzi wa maghorofa ya madarasa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi

Chalamila aagiza ujenzi wa maghorofa ya madarasa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila Chalamila ameagiza halmashauri zote kuweka mpango wa kudumu wa ujenzi wa maghorofa ya madarasa, kutokana na uhaba wa maeneo na kuboresha miundombinu ya shule ili kukabiliana na ongezeko kubwa la wanafunzi linalotarajiwa katika miaka ijayo.

Amesisitiza kuwa kukaa chini kwa wanafunzi si tatizo la fedha bali ni ukosefu wa mipango madhubuti, akitaka viongozi wa elimu kuwa na makadirio ya angalau miaka mitano hadi kumi na tano yajayo.

Akizungumza leo Februari, 12 2026 alipofanya ziara ya kutembelea Mradi wa Shule ya Sekondari Tarimba Abbasi iliyopo Tandale Chalamila amewapongeza wananchi, diwani na mbunge kwa ushirikiano mkubwa uliofanikisha ujenzi wa madarasa mapya.

“Mafanikio haya ni matokeo ya uchapakazi na mshikamano wa viongozi na jamii, hali iliyochochea maendeleo ya sekta ya elimu katika eneo hili. ifikapo mwaka 2040 idadi ya watu itaongezeka maradufu huku ardhi ikibaki ile ile, hivyo miji inalazimika kujenga majengo ya ghorofa ili kutumia nafasi ndogo kwa ufanisi,”amesema.

Kuhusu rasilimali fedha, mkuu wa mkoa aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kukusanya mapato ipasavyo na kufunga mianya ya upotevu wa kodi na fedha za ndani zinatosha kuwekeza kwenye elimu kama zitakusanywa kwa nidhamu, akihimiza pia sekta binafsi kushiriki kupitia uwekezaji wa kijamii.

Katika kuboresha ustawi wa wanafunzi, Chalamila ameagiza kuimarishwa kwa miundombinu ya mabweni na usafiri ili kupunguza changamoto za wanafunzi kuchelewa kufika nyumbani au kukosa usalama na wanafunzi wengi hukosa muda wa kusoma kutokana na umbali na usumbufu wa daladala, jambo linalochangia kushuka kwa ufaulu.

Pia amehimiza shule kushirikiana katika matumizi ya viwanja vya michezo ili wanafunzi wapate mazoezi ya kutosha kwa ajili ya afya zao. Alionya kuwa ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu linaweza kuongezeka iwapo watoto hawatazoea michezo tangu wakiwa shuleni.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Khanifa Hamza ameeleza kuwa ongezeko la wanafunzi limechangiwa na sera ya elimu bila malipo, hali inayoongeza uhitaji wa madarasa na walimu zaidi.

Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarimba Abbas, Agrey Lucas amesema mradi wa ujenzi wa shule hiyo unagharimu shilingi bilioni 3.3 mradi huo unafadhiliwa na serikali kupitia mradi wa SEQUIP na fedha kutoka mapato ya ndani.

“Mradi huu wa ujenzi wa gorofa wa Shule ya Sekondari Tarimba Abbas mradi unajumuisha ujenzi wa madarasa 21, maabara tatu, maktaba moja, matundu ya Choo 44 chumbani cha kompyuta kimoja na jengo moja la administration block,”ameeleza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here