▪Asisitiza Tanzania itaendelea kuwa kituo bora cha ushirikiano wa kikanda na Afrika
▪Asema shilingi bilioni 18.5 zimetengwa kwa ajili ya uanzishaji wa huduma za PET-CT Scan na mashine ya Cyclotron
▪Asema Tanzania inalenga kupunguza vifo vitokanavyo na saratani kwa angalau asilimia 30 ifikapo mwaka 2030
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Afrika haiwezi kushinda vita dhidi ya saratani ikiwa kila nchi itafanya kazi peke yake.

Amesema kuwa ili kufikia malengo ya mapambano dhidi ya saratani, kunahitajika kuwepo kwa ushirikiano wa kikanda na wa bara zima katika utafiti, mafunzo, kubadilishana wataalamu na kubadilishana rasilimali, teknolojia pamoja na uzoefu.
Ametoa wito huo leo Alhamisi Februari 12, 2026 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 30 ya Taasisi ya Saratani Ocean Road, yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi zote za Afrika na kupitia Taasisi ya Saratani Ocean Road tutaendelea kuwa kituo cha ushirikiano wa kikanda na bara zima katika mapambano dhidi ya saratani,”amesema.
Amesema kuwa kupitia simulizi za machapisho ya kitafiti na sayansi ambazo wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road na Tanzania kwa ujumla wameyafanya, yamekuwa na mchango mkubwa ndani na nje ya nchi kisera na kiutendaji katika mapambano dhidi ya saratani.

Katika hatua nyingine Dk. Mwigulu ameiagiza Wizara ya Afya kuandaa mkakati madhubuti wa kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa saratani ili kupunguza athari kwa rasilimaliwatu, uchumi na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
“Kutokana na tahadhari ya wataalamu wa afya kutoka Shirika la Afya Duniani kuhusu ugonjwa wa saratani kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 ifikapo mwaka 2030, Wizara ya Afya mnapaswa kuandaa mikakati ya kupunguza idadi ya wagonjwa wapya,”amesema.

Pia amesema kuwa Serikali kwa kutambua athari za ugonjwa wa saratani kwa ustawi wa nguvukazi ya Watanzania, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka mifumo mizuri ya kisera, kutekeleza mipango na mikakati muhimu dhidi ya ugonjwa huo.
“Serikali kwa kutambua athari za ugonjwa wa saratani kwa ustawi wa nguvukazi ya Watanzania imeimarisha wigo wa upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani za aina mbalimbali ikiwemo; saratani ya mlango wa kizazi, matiti, tezi dume na utumbo hadi katika ngazi ya msingi,”ameeleza.

Kwa Upande wake Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa afya si huduma pekee, bali afya ni haki, heshima, na ni ndoto za familia kwani mapambano dhidi ya saratani ni agenda ya Taifa si mzigo kwa mtu mmoja.
“Maendeleo ya kweli hayapimwi kwa maneno bali kupata huduma kwa karibu, haraka na usawa, katika eneo la saratani, tumaini hili linaonekana kwenye kasi ya maboresho ya mifumo na utoaji huduma, uongozi wa Rais Dkt. Samia umeifanya afya kuwa ni ajenda ya Taifa na tutaendelea kuleta faraja kwa Watanzania kwenye sekta ya afya,”amesema.



