Home KITAIFA chalamila: udanganyifu wachochea migogoro ya ardhi Dar

chalamila: udanganyifu wachochea migogoro ya ardhi Dar

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema migogoro mingi ya ardhi Dar es Salaam inachangiwa na tamaa, udanganyifu na matumizi ya watu wanaojifanya mawakili au madalali wanaowapotosha wananchi kwa lengo la kujipatia fedha  jambo linalochelewesha haki kupatikana.

Hayo amebainisha leo Februari, 13 2026 jijini Dar es Salaama Chalamila wakati ziara ya kikazi ya kusukiliza changamoto na kero za Wananchi katika kata kadhaa za Manispaa ya Kinondoni ikiwa lengo ni kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili, hususan migogoro ya ardhi na upatikanaji wa huduma za jamii.

Amesema ziara hizo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kusikiliza kero zao moja kwa moja badala ya kutegemea taarifa za maandishi pekee.

“Ofisi yangu iko wazi kwa wananchi wote na kwamba sitahofia kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayebainika kuvunja sheria au kunyang’anya haki za wengine na haki lazima itendeke bila kujali mtu ni nani au ana nafasi gani katika jamii na baadhi ya viobgozi wamekuwa matapeli  kushindwa kuwasaidia wananchi mnafanya kwa manufaa yenu,”amesema.

Chalamila amewaonya wananchi kuacha tabia ya kujiona wanyonge mbele ya sheria, akisema kila Mtanzania ana haki sawa bila kujali ana uwezo mkubwa wa kifedha au la, na kwamba vyombo vya dola vipo kwa ajili ya kuwatumikia wote kwa usawa.

Ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuandaa orodha ya migogoro mikubwa ya ardhi ili ichunguzwe na kutatuliwa kwa haraka, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kumiliki hati miliki za viwanja ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

Ameongeza kuwa kazi ya Baraza la Kata  ni kushauri na sio kuhukumu ni muhimu mabaraza hayo kupewa semina za kisheria mara kwa mara ili kuweza kuwasaidia wananchi katika masuala ya ardhi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea wananchi miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, kituo cha afya na mahakama ya mwanzo katika maeneo ya Nyakasangwe na Madale.

Naye Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam, Shukran Kyando amesema chanzo cha migogoro ya ardhi ni huku ngazi za chini hivyo wanapaswa kushirikiana kati ya serikali za mitaa na wizara ya ardhi.

Naye Meya wa Manispaa ya Kinondoni amesema upimaji wa viwanja katika maeneo hayo ulifanyika tangu mwaka 2017 na kampuni binafsi, lakini changamoto iliyopo ni wananchi wengi bado hawajapata hati miliki, hali inayochochea migogoro ya muda mrefu.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Wazo, Grace Mkumbwa, ameomba wakandarasi kukamilisha miradi ya barabara kwa wakati na kuhakikisha taa za barabarani zinawekwa kwa ajili ya usalama, akisisitiza kuwa miundombinu bora na upatikanaji wa hati miliki ni msingi wa maendeleo ya wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here