Home KITAIFA Kilombero Sugar yaendelea kukuza mpango wa uwezeshaji wa TEHAMA kwa manufaa ya...

Kilombero Sugar yaendelea kukuza mpango wa uwezeshaji wa TEHAMA kwa manufaa ya wanafunzi 2,500 katika Bonde la Kilombero

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

KAMPUNI ya Sukari Kilombero imekamilisha kwa mafanikio Awamu ya Pili ya Mpango wa Uwezeshaji wa TEHAMA kwa Shule, mpango endelevu unaoendeshwa na dhamira ya kampuni katika kujenga jamii inayostawi na iliyo tayari kidijitali ambapo mpango huwo unalenga kuipatia shule za sekondari zinazozunguka kampuni vifaa muhimu vya TEHAMA na ujuzi wa kiteknolojia utakaowaandaa wanafunzi katika nyanja ya teknolojia.

Akizungumza mapema leo Februari 13, 2026 katika hafla ya makabidhiano Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amepongeza hatua hiyo yenye lengo la kuboresha elimu ya Tanzania huku akiwata watendaji wa elimu kuingiza matumizi ya TEHAMA kwenye ufundishaji.

“Serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa walimu na watendaji wa elimu katika kuingiza matumizi ya TEHAMA kwenye ufundishaji na uendeshaji wa shule. Tunahamasisha wadau zaidi kuungana na Kilombero Sugar katika kuunga mkono mageuzi ya kidijitali nchini,”amesema.

Mkurugenzi wa Masuala ya Uhusiano wa Kampuni kilombero sugar, Derick Stanley, amesema kuwa mpango huu unaendana na vipaumbele vya taifa, ikiwemo dira ya maendeleo ya taifa 2050 na Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali 2024/25–2029/30 na Mwongozo wa Taifa wa Utekelezaji wa Akili Bandia katika Elimu.

Hata hivyo, kupitia Awamu ya Pili, Kampuni ya Sukari Kilombero imefanikiwa kutoa zaidi ya kompyuta za mezani (desktop) 50 zikiwa kamili kwa Shule za Sekondari za Kidodi, Iwemba na Malecela ambapo amesema lengo ni kubadilisha mazingira ya elimu nchini kwa kuongeza upatikanaji wa fursa za kujifunza kwa njia ya kidijitali.

Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa wadau, Victor Byemelwa ameeleza kuwa mpango huu uliozinduliwa Agosti 2025 utafanyika kwa awamu, na utakuwa na mfumo endelevu wa ufuatiliaji ili kuhakikisha matokeo na maboresho yatakayochochea kujifunza.

Aidha mwanafunzi wa Kidato cha Tatu kutoka Shule ya Sekondari Iwemba,Restuta Ngaema,  alionyesha furaha yake akibainisha kuwa upatikanaji wa kompyuta utamwezesha kufuatilia ndoto yake ya kuendeleza masomo ya TEHAMA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here