Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amewaongoza Mawakili wa Serikali kutoa huduma za ushauri wa Kisheria kwa wananchi wakati wa Kliniki ya Sheria bila malipo.

Huduma hiyo imelenga kuwasaidia wananchi kupata ufafanuzi na mwongozo wa masuala mbalimbali ya kisheria ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, masuala ya ndoa na familia, mikataba, pamoja na haki na wajibu wa kisheria kwa ujumla.
Timu ya Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imezinduliwa leo Februari, 16 3026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam mepiga kambi kutoa huduma mbalimbali za kisheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kuanzia tarehe 16 hadi 22 Februari, 2026.
Kupitia kliniki hiyo, wananchi wamepata fursa ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa wanasheria wa Serikali na kupatiwa ushauri wa kitaalamu, hatua inayochangia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji wa haki kwa wote.
Johari amemuhudumia mwananchi aliyekuja kupata huduma ya ushauri wa kisheria ambapo alimsikiliza na kumuhudumia Sarah Mohamed aliyewasilisha malalamiko yake kuhusiana changamoto ya mirathi inayomkabili.

“Tumeyapokea malalamiko yako na mimi pamoja na timu tutayafanyia kazi kwa haraka ili kuweza kutatua changamoto inayokukabili,”amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Katika zoezi hilo la kutoa huduma kwa wananchi Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliambatana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba na viongozi wengine.
Kliniki hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha utawala wa sheria na kuleta huduma za kisheria karibu zaidi na jamii.



