Home KITAIFA CUF yapinga uamuzi wa Msajili kutengua matokeo ya uchaguzi wa viongozi...

CUF yapinga uamuzi wa Msajili kutengua matokeo ya uchaguzi wa viongozi wakuu

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeelezea kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini wa kutengua matokeo ya uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama uliofanyika mwaka 2024, kikidai kuwa uamuzi huo una dosari za kisheria na unakiuka kanuni ya haki ya asili.

Akizungumza leo Februari, 17 2026 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Kaimu Katibu Mkuu wa chama, Magdalena Sakaya, amesema Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) lilitumia mamlaka yake ya kikatiba na kikanuni kufanya marekebisho ya muda kwenye baadhi ya kanuni ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na kuleta mshikamano ndani ya chama.

Katika uchaguzi huo, Mkutano Mkuu ulimchagua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa, Mabrouk Seif Salum kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar na Othman Dunga kuwa Makamu Mwenyekiti Bara, pamoja na kuchagua wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Kanuni Zilizotenguliwa Kwa mujibu wa Sakaya, BKUT lilitengua kwa muda kanuni tatu muhimu: Kanuni ya kuchuja wagombea na kubakisha wasiozidi watatu kwa kila nafasi ya juu;

Kanuni ya 7.1.4 inayomtaka mshindi kupata zaidi ya nusu ya kura halali;Kanuni inayohusu muda wa wagombea kujieleza na idadi ya maswali ya kuulizwa.

Amesema hatua hiyo ililenga kuruhusu wagombea wote waliokidhi vigezo kushiriki moja kwa moja kwenye Mkutano Mkuu na mshindi kupatikana kwa kura nyingi zaidi.

Malalamiko kwa Msajili

Baada ya uchaguzi huo, wanachama kadhaa wakiongozwa na Maftah Nachuma waliwasilisha malalamiko Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakipinga matokeo, wakidai kuwa washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali.

Hata hivyo, CUF imehoji muda wa kutolewa kwa uamuzi huo, ikisema malalamiko hayo yaliwasilishwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita lakini uamuzi umetolewa Februari 13, 2026.

Hoja Dhidi ya Uamuzi

Sakaya amesema katika maamuzi yake, Msajili alikiri kuwa BKUT lina mamlaka ya kisheria kutengua kanuni zake. Aidha, alikubali kupokea muhtasari wa kikao cha BKUT kilichoandaa Mkutano Mkuu huo, ambao ulisainiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Profesa Lipumba, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama wakati huo.

Hata hivyo, chama kinadai Msajili alitupilia mbali maudhui ya muhtasari huo kwa hoja kwamba haukuakisi kilichojadiliwa kikaoni, licha ya kukosa ushahidi wa moja kwa moja kwani hakukuwa na mwakilishi wa ofisi yake katika kikao hicho.

CUF pia imeeleza kushangazwa na hatua ya Ofisi ya Msajili kuanza kutoa ratiba ya uchaguzi wa marudio, ikisema jukumu la kuandaa na kusimamia uchaguzi wa ndani ya chama ni la vyombo vya chama husika kwa mujibu wa katiba na kanuni zake.

Haki ya Asili Yatajwa Kukiukwa

Kwa mujibu wa Sakaya, uamuzi wa kutengua matokeo ya viongozi wakuu watatu ulifanywa bila kuwapa fursa ya kusikilizwa kabla ya uamuzi kutolewa, jambo ambalo chama kinasema ni ukiukwaji wa kanuni ya haki ya asili (principle of natural justice) inayolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema viongozi walioguswa na uamuzi huo hawakupewa nafasi ya kujitetea juu ya tuhuma zilizowasilishwa dhidi yao, hali ambayo CUF inaitafsiri kama upendeleo na matumizi ya viwango tofauti katika maamuzi ya Ofisi ya Msajili.

Hatua Zinazofuata

CUF imesema itachukua hatua stahiki za kisheria kupinga uamuzi huo na kusisitiza kuwa itaendelea kulinda uhuru wa chama na misingi ya demokrasia ya ndani.

“Tunasimamia misingi ya haki, uwazi na utawala wa sheria. Hatutakubali taratibu za chama kupindishwa kwa maamuzi yasiyozingatia haki za msingi,” amesema Sakaya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here