Home KITAIFA Fedha za miradi zitumike kama ilivyokusudiwa-Dk. Mwigulu

Fedha za miradi zitumike kama ilivyokusudiwa-Dk. Mwigulu

Aonya watendaji wa Serikali “kuzoea” matatizo ya wananchi

Azindua mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni

Na Mwandishi Wetu, Tanga

WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa anataka kuona kila fedha inayotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo inatumika kama ilivyokusudiwa.

Amesema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wa Serikali wenye dhamana wanashindwa kufuatilia matumizi ya fedha na kusababisha kushindwa kutekelezwa kwa miradi kwa viwango na ubora kwa manufaa ya wananchi.

Amesema hayo leo Jumanne Februari 17, 2026 alipokuwa anazungumza na wananchi baada ya kuzindua mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

Mradi huo ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 526.8 una uwezo wa kuzalisha mitungi 120 ya kilo 50 kwa siku, hivyo kuboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma hii muhimu.

Mitambo hiyo imeiwezesha Halmashauri kutolazimika kusafirisha mitungi ya oksijeni hadi Jijini Tanga umbali wa takribani kilometa 175 kwa ajili ya ujazaji. Hadi sasa, mtambo umefanikiwa kuzalisha mitungi 1,440 ya hewa tiba (oksijeni) ya kilo 50 na Mitungi 200 ya kilo 15.

Aidha, Waziri Mkuu amewasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha kutekeleza majukumu yao ipasavyo na si vinginevyo. “Tunataka watu wasilale ofisini, ninyi ni watumishi wa Serikali, fedha zikiletwa zikafanye kazi iliyokusudiwa.”

Amesema hayo wakati akihoji kuhusu kukosekana kwa ubora na viwango vya majengo, risiti za malipo, kutofanyika kwa kodi ya zuio, kukosekana kwa cheti cha ubora wa mabati, matofali na saruji katika baadhi ya shule za msingi wilayani humo.

Waziri Mkuu ameonya tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuwa na utaratibu wa kuzoea matatizo ya wananchi. “Wapo baadhi ya watendaji wa Serikali wanapokea matatizo ya wananchi kama salamu na badala yake matatizo yanalimbikizwa sana.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here