Home KITAIFA Umeme ni kupaumbele katika maeneo ya uchimbaji madini-Das Kahama

Umeme ni kupaumbele katika maeneo ya uchimbaji madini-Das Kahama

📌Afungua kikao kazi kati ya TANESCO na Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Msalala

📌Aipongeza TANESCO kwa kuwashirikisha Madiwani utekelezaji wa miradi ya umeme

Na Mwandishi Wetu, Kahama

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, Glory Absalum, amesema kuwa nishati ya umeme ni muhimu na inapaswa kupewa kipaumbele katika maeneo ya uchimbaji wa madini kufuatia mchango wake katika kufungua fursa za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya maeneo husika pamoja na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi kati ya TANESCO na madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Februari 16, 2026, Katibu Tawala huyo ameipongeza TANESCO kwa utaratibu wake wa kuwashirikisha madiwani kuhusu maendeleo ya miradi ya umeme na kazi zinazofanywa na Shirika kwa kuwa madiwani ni wawakilishi wa wananchi katika maeneo yao, hivyo ni rahisi kupeleka taarifa moja kwa moja.

Aidha, amesema licha ya kazi kubwa inayoendelea kufanywa na TANESCO katika kufikisha umeme kwenye maeneo ya uchimbaji, bado kuna haja ya kuhakikisha taasisi mbalimbali kama zahanati na shule zinafikiwa na huduma hiyo muhimu.

“Ninachukua nafasi hii kuipongeza TANESCO kwa kazi nzuri ya kufikisha umeme katika maeneo ya uchimbaji. Hapa Msalala, shughuli kubwa ni uchimbaji wa madini na faida zake zimeonekana wazi. Utaratibu huu wa kuwashirikisha madiwani ni hatua nzuri inayosaidia pia kubainisha maeneo mengine ya kipaumbele katika kufikisha huduma ya umeme,” amefafanua Glory.

Naye Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Antony Tarimo, amesema kuwa TANESCO imetekeleza miradi ya kimkakati, ikiwemo upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme vya Bulyanhulu na Buzwagi, ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.

“Mahitaji ya umeme yamekuwa yakiongezeka sambamba na kukua kwa shughuli za kiuchumi. Hata hivyo, tayari tumetekeleza miradi ya kimkakati ya upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme vya Bulyanhulu na Buzwagi ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika,” amesisitiza Mhandisi Tarimo.

Baadhi ya madiwani wameishukuru TANESCO kwa kuwashirikisha , hususani utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo wamesisitiza hatua hiyo itawasaidia kufikisha taarifa kwa wananchi, hasa pale wanapohitaji ufafanuzi katika mikutano ya hadhara.

Haya yanajiri ikiwa ni muendelezo wa jitihada za TANESCO za kufanya mikutano inayowakutanisha madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na watendaji wa kata, kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu maendeleo ya miradi ya umeme katika maeneo yao, ulinzi wa miundombinu ya umeme, matumizi sahihi ya umeme pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here