Home KITAIFA NEMC yapokea gari la maabara tembezi ya kisasa yenye thamani ya...

NEMC yapokea gari la maabara tembezi ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 715

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limepokea gari lenye maabara tembezi ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni 715, hatua inayotarajiwa kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya gari hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, amesema upatikanaji wa maabara hiyo ni mafanikio makubwa katika juhudi za kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kuongeza ufanisi wa ukaguzi.

Amesema maabara hiyo imenunuliwa kupitia mradi wa miaka mitatu uliofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida), uliolenga kujenga uwezo wa taasisi za serikali na binafsi katika kusimamia mazingira.

“Mradi huo ulioanza mwaka 2020 na unaotarajiwa kukamilika Juni mwaka huu, umewezesha upatikanaji wa miundombinu muhimu ikiwemo maabara hiyo inayotoa majibu ya papo kwa papo (real time) wakati wa ukaguzi wa mazingira,” amesema.

Amesema kifaa hicho kitapima viwango vya kelele, mitetemo, ubora wa maji, hali ya hewa, udongo pamoja na metali nzito kama zebaki, hivyo kurahisisha utoaji wa maamuzi ya haraka dhidi ya vitendo vya uchafuzi wa mazingira.

“Matumizi ya maabara hii yatapunguza gharama na muda uliokuwa ukitumika kusafirisha sampuli kwenda maabara nyingine zilizoidhinishwa, ambapo gharama ya kipimo kimoja ilikuwa inaweza kufikia kati ya shilingi milioni 5 hadi 10 kulingana na aina ya sampuli,”ameeleza.

Amesema kwa sasa NEMC itaweza kufanya uchunguzi ndani ya muda mfupi na kuchukua hatua stahiki mara moja, hali itakayoongeza ufanisi katika kulinda mazingira.

Dk.Semesi amesema baraza lina kanda 13 nchini na matarajio ni kupata angalau magari 12 zaidi ya maabara tembezi ili kuimarisha huduma katika mikoa yote na kuhakikisha ukaguzi unafanyika kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Naye Mratibu wa Mradi huo, Paul Kalokola, amesema maabara hiyo pia ina vifaa vya kisasa ikiwemo droni kwa ajili ya kufikia maeneo magumu na yaliyofichika, hatua itakayowezesha upimaji wa kisayansi kufanyika popote nchini na kusaidia maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kitaalamu.

Kwa upande wake Meneja wa Programu za Nishati Mazingira na Hali ya Hewa kutoka Ubalozi wa Sweden, Stephen Mwakifwamba
amesema serikali ya Sweden imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi.

Amesema jumla ya mradi huo ulikuwa na thamani ya dola milioni tatu za Marekani na ulijumuisha pia uboreshaji wa sheria na kanuni za mazingira pamoja na kuzitafsiri kwa Kiswahili ili ziweze kueleweka kwa wananchi.

Aidha ameishauri NEMC kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ili viweze kudumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here