Home KITAIFA Kamati ya bunge ya Nishati na Madini yaridhishwa na hali ya uzalishaji...

Kamati ya bunge ya Nishati na Madini yaridhishwa na hali ya uzalishaji umeme

📌Yasema jumla ya megawati 4,400 za umeme zinazalishwa kupitia vyanzo mbalimbali

📌Yaipongeza TANESCO kwa kutekeleza Miradi na kuhakikisha Shirika linajiendesha kwa faida

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema imeridhishwa na hali ya uzalishaji wa umeme , ambapo sasa nchi ina uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 4,400 huku matumizi yakiwa ni megawati 2,071 hatua ambayo imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme.

Hayo yamejiri Februari 20,2026 baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya kukagua miradi ya umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo imetembelea Kituo cha Kusafirisha Umeme kwenda Zanzibar cha Ras Kilomoni na Kituo cha kuzalisha Umeme kwa Gesi Asilia cha Kinyerezi I na II.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema kumekuwa na maendeleo makubwa katika eneo la uzalishaji wa umeme, na sasa TANESCO inaendelea na jitihada za kujenga njia za kusafirisha umeme, ikiwemo ya kutoka Bwawa la Julius Nyerere hadi Chalinze, kisha Kinyerezi hadi Mkuranga, eneo lenye viwanda vingi vya uzalishaji.

“Tunaipongeza sana TANESCO kwa utekelezaji wa miradi ya umeme. Ile hali ya kukatika kwa umeme imepungua, na sasa hakuna mgao. Kamati inashauri kuwa nguvu kubwa sasa itumike katika kuhakikisha umeme unamfikia mlaji wa mwisho, hususani katika maeneo ya viwanda na migodi,” amefafanua Subira.

Naye Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Innocent Luoga, amesema wamepokea maagizo ya Kamati kuhusu maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 nchi iweze kuzalisha jumla ya megawati 8,000.

“Hivi sasa mahitaji ya umeme yameendelea kuongezeka, hasa katika shughuli za uzalishaji. Serikali kupitia TANESCO, inahakikisha umeme unawafikia wananchi, na lengo ni kuwaunganishia umeme takribani wananchi milioni 1.7 kwa mwaka,”amesema.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilianza ziara yake katika Kituo cha Kusafirisha Umeme kwenda Zanzibar cha Ras Kilomoni, chenye uwezo wa kusafirisha jumla ya megawati 205, ambapo kwa rekodi ya mwaka 2025 mahitaji ya Zanzibar yalikuwa ni megawati 140.4.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here