Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
VITUO sita vya kilimo ikolojia hai nchini, vinavyotekeleza Mradi wa AgroKilimo, vimekutana katika warsha ya siku tatu kwa ajili ya kuchanganua na kujadiliana namna ya kuendeleza kilimo hicho kwa wakulima.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shiriki la Islands of Peace (IDP), Ayesiga Buberwa wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa warsha hiyo ya siku tatu iliyofanyika kwenye Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Hai (SJS) Kwanyange wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Buberwa alisema Mradi wa AgroKilimo unafadhiliwa na Serikali ya Ufaransa kwa Euro laki 515 kwa miaka miwili, umechagua vituo sita vya majaribio ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kujenga mustakabali imara na endelevu wa kilimo hicho
“Mpango huu unalenga kuimarisha vituo vya majaribio kote nchini. Kwa msaada wa Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, mradi huu unalenga kujenga ujuzi, kusambaza maarifa, na kuunda mtandao thabiti wa kitaifa wa vituo vinavyokuza ubunifu katika kilimo ikolojia,” amesema.
Mkurugenzi huyo ameyataja mashirika yanayoenda kunufaika na Mradi wa AgroKilimo ni IDP, Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) Morogoro, Practical Permaculture Institute of Zanzibar (PPIZ) Zanzibar, St. Joseph Sustainable Organic Farm (SJS) Kilimanjaro, Research, Community and Organizational Development (RECODA), Arusha, Mogabiri Farm Extension Center (MFEC) na Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima Bihawana Dodoma.

Pia mradi huu utafadhili utafiti wa Shahada ya Uzamili kwa wanafunzi wanaosoma Kilimo Ikolojia Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na kushirikiana kwa karibu na Kitovu cha Kilimo Ikolojia Tanzania (AEHT), ambacho ni kitovu kikuu cha utafiti wa mradi, kikiunganisha washirika wote wa kilimo hicho katika masuala ya utafiti.
Amesema katika warsha hiyo, kila kituo kilipitia vipengele muhimu vya kazi zake, ikiwemo historia yake, muundo wa shirika, mbinu za utafiti na mafunzo, miundombinu na vifaa, usimamizi wa wafanyakazi, bajeti na mifumo ya ufadhili, ulinganifu na mfumo wa Wizara ya Kilimo, pamoja na mipango ya muda mrefu ya uendelevu.
Amesema Mradi wa Agro Kilimo ulizinduliwa mwaka 2025 na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne-Sophie Avé ambapo mradi umejengwa katika nguzo kuu mbili.
Amesema nguzo ya kwanza ni kufanya na kuthibitisha tathmini shirikishi ya namna vituo vya kilimo ikolojia vinavyoendeshwa nchini Tanzania.

“Nguzo ya pili ni kuandaa njia za vitendo za kuviwezesha vituo kuunganishwa katika mtandao pamoja na kuunda miongozo ya pamoja ya utafiti, maendeleo, na mafunzo.
Hiyo inajumuisha utafiti wa matumizi na utafiti wa ulinganishaji wa mazao katika mazingira tofauti, kuwashirikisha wakulima katika shughuli za utafiti, mbinu shirikishi za ugani, na mifumo endelevu ya mafunzo ya kitaaluma.
Buberwa amesema kupitia warsha hiyo wamebaini changamoto kadhaa ikiwemo vituo vingi kuwa na uhaba wa wataalamu kutokana na bajeti ndogo na nyingine nyingi, hivyo wataenda kufanyia kazi.
Akizungumzia warsha hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa PPIZ, Ikram Ramadhan Soraga amesema mradi huo umekuja wakati muafaka na utenda kuleta mabadiliko ya kilimo ikolojia hai Zanzibar.
Soraga amesema matamanio ya PPIZ ni kuona Zanzibar na dunia kwa ujumla inatumia vyakula vinavyotokana na uzalishaji wa mifumo ya kilimo ikolojia hai kwa kuwa ina faida kiuchumia, kiafya na mazingira.
Naye Felician Pius wa SJS, amesema ujio wa mradi wa AgroKilimo ni muhimu kwao kwani dhamira yao ni kuirejesha sekta ya kilimo kwenye mfumo wake wa zamani ambao ni salama.
Kiongozi wa Program wa RECODA amesema Mradi wa AgroKilimo kupitia IDP umeweza kuwabadilisha hasa kwenye eneo la muundo wa shirika lao, ili kuweza kupata matokeo chanya kwa haraka.
Meneja Msaidizi wa MFEC, Peter Mwita amesema mradi huo unaenda kuendeleza mapambano yao kwenye eneo la kilimo ikolojia, ikiwemo kuboresha miundombinu ikiwemo uvunaji wa maji na mengine.



