Home KITAIFA Polisi: Tumeshtushwa na taarifa za mchungaji kutekwa

Polisi: Tumeshtushwa na taarifa za mchungaji kutekwa

Na Mwandishi Wetu

JESHI la Polisi limesema limeshtushwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni zikidai kuwa Mchungaji Yanick Mbombo Cele, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ametekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, mchungaji huyo aliwahi kukamatwa Mei 15, 2025 mkoani Iringa kwa tuhuma za ubakaji na mauaji ya watoto wadogo. Hata hivyo, baada ya uchunguzi kufanyika, ushahidi wa tuhuma za mauaji na ubakaji haukukidhi vigezo vya kumfungulia mashtaka.

Polisi wameeleza kuwa uchunguzi pia ulibaini kuwa alikuwa akiishi nchini kinyume cha sheria. Juni 17, 2025 yeye na wenzake watano walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kuendesha genge la uhalifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika kesi namba ECO 00014959/2025.

Aidha, Julai 14, 2025 watuhumiwa walikiri makosa yao kupitia makubaliano ya kisheria (plea bargain), wakalipa faini ya shilingi milioni 20 kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na magari yao kutaifishwa.

Polisi wameeleza kuwa baada ya hukumu hiyo, ilibainika kuwa mchungaji huyo aliendelea na vitendo vya udanganyifu kupitia kanisa lake la Ebenezer Restoration Ministry for All Nations ambapo aliwalipa pesa baadhi ya waumini wake ambao walijifanya wagonjwa na wengine kujifanya ni walemavu ili wafike kanisani kwake kwa maombi na kujifanya kuwa wamepona huku wangine wakijifanya kupiga simu za ushuhuda wa kuponywa

Taarifa ya polisi imeeleza kuwa mchungaji huyo alikamatwa tena na Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi mkoani Iringa na kukabidhiwa kwa Kamanda wa Uhamiaji wa Mkoa huo, ambapo aliondolewa nchini na kupigwa marufuku kurejea.

Jeshi la Polisi limesema linashangaa kuona taarifa zikidai mchungaji huyo yupo nchini na ametekwa. Polisi wamesema wanaendelea kuchunguza madai hayo na wametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa sahihi au ushahidi kuwasiliana na kituo cha Polisi kilicho karibu naye.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here