Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam.
SERIKALI imesema Mkutano wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache (Minority Interests Forum-MIF 2026) utakuwa jukwaa mahususi la kujadili, pamoja na mambo mengine, mikakati ya kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.

Mkutano huo, unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), utafanyika kuanzia Machi 16 hadi 18, 2026 katika Ukumbi wa PAPU, jijini Arusha, na unatarajiwa kuwakutanisha Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu kati ya 150 na 200 kutoka kampuni 56 ambazo Serikali inamiliki hisa chache, yaani chini ya asilimia 51.
Akizungumza leo Februari, 24 2026 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini – Mashirika ya Kibiashara, Lightness Mauki, alisema kuwa safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu si ya kubahatisha, bali ni matokeo ya maamuzi ya kimkakati, usimamizi thabiti na uongozi unaotazama mbele.
“Tunakwenda kujadili namna ya kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia ili tuweze kufikia lengo la uchumi wa kati wa juu katika kipindi cha miaka 24 ijayo kama ilivyobainishwa kwenye Dira 2050,” amesema Mauki.
Alieleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kutoka ufuatiliaji na usimamizi wa kawaida kwenda katika uongozi na usimamizi unaoangalia mbele” inalenga kuhamasisha mageuzi ya fikra kutoka ufuatiliaji wa kawaida wa utendaji kwenda katika uongozi bunifu na unaotazama mbele, unaotambua mapema vihatarishi na kutumia fursa za kimkakati katika mazingira ya mabadiliko ya haraka ya kiuchumi na kiteknolojia.
Tanzania imejiwekea lengo la kimkakati la kukuza uchumi wake kutoka takriban dola za Marekani bilioni 85 hadi kufikia dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 kupitia utekelezaji wa Dira 2050, inayolenga kujenga uchumi wa juu wa kati, wenye ushindani na jumuishi.
Amesisitiza kuwa kufikia lengo hilo kunahitaji kuachana na usimamizi wa kimazoea na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
“Tunahitaji usimamizi ambao si wa kimazoea na lazima tufanye kazi kwa kushirikiana na sekta binafsi,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali na mipaka ya nchi kwa wivu mkubwa ili kuhakikisha uwekezaji unaingiza thamani halisi kwa Taifa.
“Lazima tulinde rasilimali na mipaka ya nchi yetu kwa wivu mkubwa,” ameongeza.
Mauki amesema OMH itaendelea kuhakikisha uwekezaji wote katika kampuni ambazo Serikali ina hisa chache unakuwa na tija, unaleta matokeo yanayotarajiwa na unaichangia Tanzania kusogea karibu zaidi na lengo la uchumi wa kati wa juu.
Kupitia jukwaa hilo, viongozi wa kampuni watajadili uoanifu wa mikakati ya taasisi zao na Dira 2050, matumizi ya teknolojia katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji, pamoja na uchambuzi wa taarifa za kiuchumi na kiushindani katika kuboresha maamuzi ya uwekezaji.
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kampuni hizo zimeendelea kuonesha mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kwa kuimarisha mapato ya Serikali kupitia kodi na gawio, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali za kimkakati.
Takwimu rasmi zinaonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hicho.
Thamani ya uwekezaji wa Serikali katika kampuni hizi imeongezeka kutoka shilingi bilioni 821.51 mwaka 2020 hadi shilingi trilioni 1.94 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 136.
Mapato ghafi yameongezeka kutoka shilingi trilioni 6.81 hadi shilingi trilioni 10.74, sawa na ongezeko la asilimia 58, huku faida ikiongezeka kutoka shilingi trilioni 1.79 hadi shilingi trilioni 1.95.
Katika kipindi cha 2020 hadi 2024, kampuni hizi zimechangia takribani shilingi trilioni 3.67 kama kodi ya mapato ya kampuni.
Aidha, gawio kwa Serikali limeongezeka kutoka shilingi bilioni 58.26 hadi shilingi bilioni 266.52, sawa na ongezeko la asilimia 357.
Kwa mtazamo wa Mauki, mafanikio hayo yanaonesha kuwa mwelekeo uliopo ni sahihi, lakini bado kuna wajibu wa kuongeza kasi, ubunifu na ufanisi katika uongozi wa kampuni hizo ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya kiuchumi ifikapo mwaka 2050.
“Tunapoelekea mwaka 2050, tunahitaji uongozi thabiti, unaotazama mbele na unaochukua hatua mapema. Huu si wakati wa kusubiri matokeo; ni wakati wa kuyatengeneza,” amesema.



