Home AFYA Tahadhari yatolewa ongezeko la maambukizi ya UVIKO-19

Tahadhari yatolewa ongezeko la maambukizi ya UVIKO-19

Na Mwandishi Wetu

WIZARA  ya Afya imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu ongezeko la magonjwa ya mlipuko yakiwemo mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, homa ya Dengue na Kipindupindu na kutoa wito kwa jamii kuzingatia kikamilifu hatua za kinga ili kudhibiti maambukizi.

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 25,2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe amesema takwimu za ufuatiliaji zinaonesha kuwa kila mwaka kati ya mwezi Novemba hadi Aprili kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali na UVIKO-19 nchini na duniani.

Amesema magonjwa hayo ya huambukizwa kwa njia ya hewa na husambaa kwa njia ya matone madogo yanayotoka kwa mtu mwenye maambukizi anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza, na yanaweza kusababisha homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua pamoja na uchovu.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Magembe amewataka wananchi kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili au wanapokaribiana na wenye dalili.

“Wizara inaonya kuhusu ongezeko la homa ya Dengue hasa katika kipindi cha mvua, ugonjwa huo huenezwa na mbu aina ya Aedes. Dalili zake ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa, viungo na macho,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kuhusu Kipindupindu, Dk. Magembe amesema licha ya nchi kuimarisha udhibiti wake na kutoripotiwa kwa takribani mwezi mmoja sasa, bado kuna hatari ya maambukizi mapya hasa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika nchi jirani.

Amesisitiza umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa au kuyatibu, kunawa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka chooni, kuosha matunda kwa maji safi, kutumia vyoo bora na kuepuka kula vyakula vilivyoandaliwa katika mazingira yasiyo safi.

Serikali imeahidi kuendelea kufuatilia mwenendo wa magonjwa hayo na kutoa taarifa mara kwa mara endapo kutatokea mabadiliko yoyote au hatua zaidi zitahitajika kuchukuliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here