Home SIASA NLD YAPULIZA KIPYENGA NAFASI ZA WAGOMBEA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU.

NLD YAPULIZA KIPYENGA NAFASI ZA WAGOMBEA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU.

Na Boniface Gideon,HANDENI

CHAMA cha National League for Democrats (NLD) ,leo kimetangaza kuanza kwa mchakato wa ndani ya chama wa kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani,ubunge na rais kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Pia Chama hicho kimetangaza neema kwa wagombea Wanawake, kuwa hawatotoa ada yoyote wakati wa kuchukua fomu,lengo ni kuwapa fursa ya kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi.

Akizungumza mapema leo Machi,2 2025 na waandishi wa Habari Katibu Mkuu wa NLD Taifa ,Doyo Hassan Doyo, amesema chama hicho kimelenga kusimamisha wagombea katika majimbo yote ya Uchaguzi kuanzia udiwani,ubunge pamoja na nafasi ya rais.

“Chama chetu kitashiriki Uchaguzi Mkuu,hivyo kwakutambua hilo,leo tunatangaza rasmi kuwa ,chama kimefungua milango ya kuanza mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na rais,hivyo watu wote wenye sifa wanakaribishwa kushiriki,ili ukidhi sifa ya kushiriki mchakato huu ni lazima uwe mwanachama hai wa Chama chetu,”amesema.

Doyo amesema kuwa, kwaupande wa wagombea Wanawake hawatolipa ada yoyote wakati wa mchakato wa kuchukua fomu.

“Chama chetu,kwa mapenzi mema kabisa,na kwakuona umuhimu wa akinamama,tumeamua kuwa , Wanawake wote watakaojitokeza kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama chetu,hawatolipa ada yoyote ya fomu,hii itasaidia kuongeza hamasa na kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za Udiwani, Ubunge na Rais,” amesema.

Ameongeza kuwa , katika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho Februari 23 mwaka huu, kilianzimia kuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu nilazima kufanyike mikutano ya hadhara na ndani ili kupata wagombea wenye uwezo pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) nilazima iweke wasimamizi wa Uchaguzi wenye weledi ili Uchaguzi uwe huru na haki.

“katika kikao chetu cha hivi karibuni,chama chetu kiliazimia kuwa ni lazima tufanye mikutano ya hadhara kwakipindi hiki ili tupate wagombea wenye uwezo,lakini pia kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi’INEC’nilazima iweke wasimamizi wa Uchaguzi wenye weledi ili Uchaguzi uwe huru na haki,na usiwe na dosari,” amesisitiza Doyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here