Dar es Salaam
MRATIBU wa Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi amesema wadau wa kilimo wana kazi kubwa ya kuhakikisha mbegu asili zinatumika kwa wingi kwenye kilimo, kwa kuwa zinazalisha mazao mengi ambayo yanaimarisha afya za watumiaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki Mkindi amesema iwapo kila mdau atakuwa anahamisha wakulima kutumia mbegu za asili ni wazi upotevu wa mbegu hizo utaanza kurejea.
“Wadau tuna kazi ya kufanya kuhakikisha mbegu za asili zinasaidia katika kuimarisha afya zetu, mtindo wa maisha wa sasa umechangia mbegu hizo kutopewa kipaumbele, lakini sisi tunaendelea na jitihada za kutoa elimu na kuhamasisha kwa wakulima kuzitumia kulinda baionuai na kuimarisha afya zao,”amesema Mkindi.
Amesema kilimo cha kutumia mbegu asili za wakulima ni endelevu na kinachangia utunzaji mazingira, kuhamasisha matumizi ya mbegu asili kwa wakulima kutambua na kuunga mkono mbegu zao kutoka enzi na enzi zikitumika.
Amesema katika kuhakikisha mbegu hizo zinapatikana kwa urahisi, wameanzisha zaidi ya benki 40 za mazao aina mbalimbali kulingana na uzalishaji wa eneo husika.
Mkindi amefafanua kuwa mbegu ndio nguzo kuu katika uzalishaji wa kilimo na mbegu zilizohifadhiwa na wakulima huchangia idadi kubwa ya usambazaji.
“Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania na kuajiri zaidi ya asilimia 65 ya watanzania kulingana na taarifa ya Wizara ya Kilimo (MOA 2023). Pia sekta hii inachangia wastani wa asilimia 26.6 kwa Pato la Taifa (GDP),”ameeleza.
Amesema hadi sasa zaidi ya wakulima 200,000 wamejengewa uwezo wa matumizi sahihi ya mbegu hizo kwa kushirikiana na mashirika zaidi ya 30 ambayo yamejikita kwenye uhamasishaji wa kilimo ikolojia hai.
Mkindi amesema pamoja na kuhamasisha wakulima kujikita kwenye kilimo cha mbegu asili, pia wanaendelea kuhamasisha serikali irekebishe sheria na sera ya mbegu ambazo kwa sasa hazitambui mbegu hizo.
“Sisi kila kukicha tunapigania mbegu asili ambazo asilimia 90 zinamilikiwa na wakulima na imani yetu ni siku moja kuona wakulima wote wanatumia mbegu hizo kwani zina faida kiuchumi, afya na mazingira. Lakini ili jitihada hizo zifanikiwe ni lazima sheria na sera ya mbegu zitambue mbegu hizo,” amesema.