Na Esther Mnyika, Kilimanjaro
Viongozi wa Serikali, mashirika ya umma na binafsi, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa kimila, vyama vya siasa, wanafunzi na wananchi kwa ujumla wamejitokeza kwa wingi kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Cleopa David Msuya.
Ibada hiyo ya kutoa heshima za mwisho imefanyika leo Mei 12, 2025 katika viwanja vya CD Msuya, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, huku ikiendeshwa kwa heshima kubwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Mwili wa Msuya uliwasili jana asubuhi saa 2:20 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ndege ya Shirika la Air Tanzania, ambapo ulipokelewa kwa heshima ya kijeshi na viongozi mbalimbali wa Serikali kabla ya kusafirishwa kuelekea Mwanga kwa ajili ya ibada na kuaga.
Baada ya ibada katika viwanja vya CD Msuya, msafara uliendelea hadi katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Kilaweni, Usangi kijijini kwao, ambapo wananchi wa maeneo ya jirani walipata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho. Hatimaye, mwili wa hayati Msuya ulipelekwa nyumbani kwake kwa maandalizi ya mazishi yatakayofanyika kesho Mei 13, 2025.

Viongozi waliohudhuria shughuli hizo ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Juma Mkomi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, na Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamza Juma, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM (SUKI) Rabia Hamid, pamoja na wabunge wa mkoa wa Kilimanjaro akiwemo Saashisha Mafuwe (Hai) na David Mathayo (Same Mashariki), miongoni mwa viongozi wengine.
Hayati Msuya alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro na alifariki dunia Mei 7, 2025 kutokana na maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho kijijini kwake Chomvu, wilayani Mwanga.