Home KITAIFA Rais Samia: Nimetimiza maombi ya Hayati Msuya kabla hajatuaga

Rais Samia: Nimetimiza maombi ya Hayati Msuya kabla hajatuaga

Na Esther Mnyika, – Kilimanjaro

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema amepata faraja ya kipekee kutimiza maombi makubwa mawili ya aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Hayati Cleopa David Msuya, kabla ya kuaga dunia—kukamilika kwa mradi wa maji Same–Mwanga–Korogwe na kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Cde Msuya Bypass.

Akizungumza leo Mei 13, 2025, wakati wa ibada ya mazishi ya kitaifa ya Hayati Msuya katika Usharika wa Usangi Kivindu, Kanisa la KKKT, Wilaya ya Mwanga, Rais Samia amesema Hayati Msuya alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu miradi hiyo na aliitaka Serikali ihakikishe inakamilika kwa manufaa ya wananchi wa Mwanga.

“Ile ndiyo miradi mikubwa aliyokuwa akiitamani sana. Mara ya mwisho tulionana wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji Mwanga. Alikuwa hawezi kutembea lakini alikuwepo kwenye kigari chake, akiwa na furaha kubwa,” amesema Rais Samia.

Hayati Msuya alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga, na alifariki dunia Mei 7, 2025, katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi ya moyo. Leo ameagwa rasmi na kuzikwa katika makaburi ya familia nyumbani kwake, Usangi.

Urithi wa mabadiliko na mshikamano

Rais Samia alieleza kuwa Msuya alikuwa mtu wa maono, asiyeogopa mabadiliko, na aliamini katika mshikamano wa kitaifa. Alisisitiza kuwa urithi wa Msuya haupo tu kwenye nafasi alizoshika, bali pia katika msimamo thabiti wa kuamini maendeleo yanapatikana kwa kujenga wataalam, umoja, na kusimamia rasilimali kwa uadilifu.

“Katika historia yake, kuanzia mwaka 1956 alipoanza kazi kama Afisa Maendeleo ya Jamii, hadi alipostaafu rasmi mwaka 2000, na baadaye 2021 alipoachia nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ardhi, alijitoa kwa ajili ya Watanzania,” amesema Rais Samia.

Aliweka rekodi ya kuwa Waziri aliyedumu kwa muda mrefu, na pia kuwa Makamu wa Rais kwa kipindi kifupi zaidi—miezi 11, kabla mfumo wa mgombea mwenza haujaanza kutumika.

Salamu za Rambirambi: Viongozi watambua ukomavu wake

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, alisema kifo cha Msuya kimeacha somo kwa taifa na kuwataka Watanzania kujifunza kutoka kwenye maisha yake ya uadilifu, ustahimilivu, na hekima.

“Alikuwa mtu aliyeaminika na viongozi wakuu wa nchi kama Mwalimu Nyerere na Rais mstaafu Mwinyi, aliweza kushughulikia changamoto hata za vita ya Idd Amin na wakati mgumu wa kiuchumi,” amesema Prof. Juma.

Askofu Dk. Alex Malasusa, aliyeongoza ibada hiyo, alimsifu Msuya kuwa mfano wa kiongozi aliyesikiliza na kunyenyekea.

“Sote tunakubaliana kuwa Mzee Msuya alikuwa kiongozi wa watu wa dini zote. Aliishi kwa upendo na alitanguliza amani. Alikuwa mtu wa hekima, busara na utulivu,” amesema Askofu Malasusa.

Jakaya Kikwete: Mwalimu na Baba

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema alifaidika mno na hekima ya Msuya, ambaye alimchukulia kama mwalimu na mshauri wake mkubwa.

“Alikuwa siyo mtu wa kawaida. Mwaka 1988 tulianza kuwa karibu, na amenilea kisiasa. Hakuwa mwepesi kulalamika au kukosoa hadharani. Alijua kila hatua ya uchumi wa taifa hili,” amesema Kikwete.

Dk. Mpango: Alitufundisha kuwa karibu na wananchi

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alisema Hayati Msuya alimuusia kuwa viongozi wanapaswa kuwafuata wananchi walipo—hata kama ni milimani.

“Alisema wapare wanaishi milimani, hivyo tuwapandie, tuwasikilize. Alikuwa kiongozi mwenye maono ya mbali,” amesema Dk. Mpango.

Mtoto Wake: Alituongoza kwa nidhamu na kujituma

Kwa niaba ya familia, Jobu Msuya, mtoto wa Hayati Msuya, alisema Baba yao aliwaasa kupambana maishani bila kumtegemea mtu.

“Sikumbuki kama baba alishawahi kunipa hata senti moja. Alisisitiza tupambane na tusimwone kama chanzo cha fedha. Alikuwa mshauri mkubwa sana,” amesema Jobu.

Alifichua kuwa Januari 4 mwaka huu, Hayati Msuya alisherehekea kwa mara ya kwanza siku yake ya kuzaliwa na kueleza ndoto yake ya kujengwa kwa chuo kikuu cha teknolojia Wilayani Mwanga, na pia kuona Hakika Bank anayoiamini ikikua hadi kuwa taasisi kubwa kama NMB au CRDB.

Wosia kwa Taifa

Katika salamu zake, Rais Samia aliwaasa viongozi wa kizazi cha sasa kuyasimamia wanayoamini bila kuyumbishwa, kuwa waaminifu, wazalendo na waadilifu, kama alivyokuwa Hayati Msuya.

“Tujifunze kuyaishi maisha yenye maadili na dhamira ya kweli ya kulijenga taifa letu. Tuendelee kuenzi busara na mchango wa viongozi wetu waasisi,” alisisitiza Rais Samia.

Mazishi haya yalihudhuriwa na viongozi wa Serikali, Bunge, Chama cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa dini, wananchi wa Mwanga na mikoa ya jirani pamoja na waombolezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here