Na Esther Mnyika, Lajiji
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imetoa onyo kali kwa vyuo na watu wote wanaojaribu kuingia kwenye taaluma ya uandishi wa habari kwa kutumia vyeti bandia au nyaraka zisizotambulika kisheria, ikisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu huo.

Onyo hilo limetolewa leo Mei 19, 2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando, wakati akitangaza kuanza kwa utoaji rasmi wa vitambulisho vya waandishi wa habari (Press Cards) kwa waandishi waliokidhi vigezo vya kitaaluma na kimaadili.
Mhando amesema kuwa baadhi ya waombaji wamekuwa wakijaribu kutumia vyeti feki ili kujipatia ithibati, jambo ambalo si tu ni kosa la kinidhamu bali pia ni kosa la jinai, na endapo watafumaniwa, watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufutiwa usajili na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Amesema Bodi haitasita kufuta usajili wa mwandishi yeyote atakayebainika kuwasilisha nyaraka za kughushi, huku akifafanua kuwa lengo la mfumo mpya wa TAI-Habari ni kuhakikisha waandishi wote wanaotambulika kitaaluma wana sifa halali na wamepata mafunzo stahiki kwa mujibu wa sheria.
“Mfumo wa TAI-Habari unalenga kurahisisha huduma kwa waandishi wa habari kwa njia ya kidijitali na kuboresha usimamizi wa taaluma hiyo kwa kuhakikisha kila mwandishi anafanya kazi kwa mujibu wa kanuni, weledi na viwango vya kitaaluma. Mhando amesema maombi ya ithibati na vitambulisho yatafanyika kupitia kiunganishi cha mtandao cha https://www.taihabari.jab.go.tz ambapo mwandishi atajisajili kwa kujaza taarifa zake, kupokea msimbo wa usajili kwa njia ya SMS na barua pepe, kujaza wasifu, kulipia ada ya ithibati ya Shilingi 50,000 kwa waandishi wa ndani au Dola 500 kwa waandishi wa kigeni, na kuwasilisha maombi yake kwa uchakataji,” amesema Mhando.
Ameeleza kuwa baada ya mchakato huo, mwombaji atapokea ujumbe wa kuthibitisha hatua ya maombi yake, na atajulishwa mahali na muda wa kuchukua kitambulisho endapo atakidhi vigezo.
Kwa mujibu wa Mhando, mahitaji muhimu ya kuambatishwa katika maombi ni pamoja na picha ndogo ya rangi (passport size), vyeti vya elimu vilivyothibitishwa na mamlaka husika kama vile TCU au NACTVET, barua ya utambulisho kutoka taasisi anayofanyia kazi au kwa waandishi wa kujitegemea (freelancers), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), pamoja na barua pepe na namba ya simu inayofanya kazi.
Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 na Kanuni ya 17 ya Sheria hiyo kupitia Tangazo la Serikali Na.18 la Februari 3, 2017, watu wanaopaswa kupewa ithibati ni pamoja na wahariri, waandishi wa habari, wapiga picha, wazalishaji wa habari na watangazaji wa redio na televisheni, huku akisisitiza kuwa wote wanapaswa kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Stashahada ya Uandishi wa Habari au taaluma inayohusiana nayo.
Mhando amehitimisha kwa kusema kuwa hatua hii inalenga kulinda heshima ya taaluma ya uandishi wa habari nchini na kuhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa kwa umma zinatoka kwa waandishi wenye ujuzi, maadili na uwajibikaji, huku akiwahimiza wanahabari kushirikiana kwa dhati na Bodi hiyo ili kuhakikisha mchakato wa usajili na utoaji wa vitambulisho unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma.