Home KITAIFA LATRA yaja na mfumo mpya wa VTS wa kufuatilia mwenendo wa daladala

LATRA yaja na mfumo mpya wa VTS wa kufuatilia mwenendo wa daladala

Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeanzisha mfumo mpya wa ufuatiliaji wa mwenendo wa daladala nchini zikiwemo zinazokatisha ruti kinyume na leseni zao.

Pia Mfumo huo unaojulikana kama VTS (Vehicle Tracking System) sasa umeanza kusimikwa rasmi kwenye magari ya abiria mijini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha huduma za usafiri zinatolewa kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Akizungumza Juni,2 2025 jijini Dodoma katika Maonesho ya Mazingira Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa LATRA, Salum Pazi amesema mfumo huo ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kuboresha mazingira na huduma kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira, ikiwa ni pamoja na usafiri unaotumia nishati safi kama vile umeme na gesi asilia.

“LATRA imekuwa ikihamasisha matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati mbadala kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa mazingira,”amesema.

Amesisitiza kuwa changamoto ya daladala kukatisha ruti imekuwa kero kwa muda mrefu, jambo ambalo sasa linaanza kudhibitiwa kupitia mfumo wa VTS.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu daladala kutozingatia ruti wanazopaswa kufuata, Kwa sasa, tumeanza kufunga mfumo wa VTS kwenye magari ya mijini ili kuhakikisha kila chombo cha usafiri kinafuata leseni iliyoidhinishwa,” amesema.

Kwa mujibu wa LATRA, ifikapo Julai mwaka huu, mabasi yote ya mijini yanatakiwa kuwa yamefungwa mfumo wa VTS ili kuhakikisha udhibiti thabiti wa utoaji huduma.

Aidha amewahimiza Wananchi wa Jiji la Dodoma kutembelea maonesho hayo ya mazingira katika banda la LATRA katika viwanja vya maonesho hayo ili kujionea kwa macho teknolojia hizi mpya na kupata elimu ya namna ya kuzitumia kwa manufaa yao.

Ameongeza kuwa LATRA imeanzisha pia Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (Passenger Advisory System – PAS) ambao unawawezesha abiria kufuatilia mabasi wanayoyasubiri kupitia anuani ya https://pas.latra.go.tz.

Amesema,kwa kutumia mfumo huu, abiria anaweza kuchagua kituo alichopo na kuona mabasi yote yanayokuja, pamoja na kufuatilia namba ya basi na kuona lilipo kwa wakati huo.

“Kwa mfano, kama unamsubiri ndugu yako anayesafiri na basi, huna haja ya kumpigia simu kuuliza yupo wapi. Unaingiza tu namba ya gari kwenye mfumo na utaweza kuona lilipo pamoja na kasi yake ya mwendo katika spidi kumi za mwisho.

Mfumo huu pia unaruhusu abiria kutoa taarifa za changamoto, kama vile mwendo kasi usio wa kawaida, kwa kupiga simu bure kupitia namba zilizopo kwenye mfumo huo,”amefafanua.

Vile vile amesema,LATRA pia inao Mfumo wa Tiketi Mtandao (Safari Ticket) – mfumo jumuishi unaowezesha abiria kufanya uhifadhi wa tiketi kwa mabasi yaendayo mikoani, treni ya SGR na ile ya reli ya kati.

Amesema,Mfumo huo umeanza kutumika rasmi mwaka huu na unalenga kurahisisha upatikanaji wa tiketi kwa njia ya kidigitali.

Katika maonesho hayo, LATRA inaonesha mfano halisi wa pikipiki ya magurudumu matatu (bajaji) inayotumia umeme – chombo kinachobeba abiria na kina uwezo wa kusafiri hadi kilomita 100 kwa chaji moja ya saa tatu.

“Hili ni moja ya jitihada za kuonesha kuwa huduma za usafiri zinaweza kutolewa bila kuchafua mazingira,” amesema Pazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here