Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewataka wateja wao kulipa madeni ya malipo ya kabla na baada ili kuweza kuboresha huduma ya umeme nchini ili iweze kuwa na tija na ufanisi kwa Taifa.

Hayo ameyasema leo Juni, 19 2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Irene Gowelle wakati akizindua kampeni ya lipa deni ,linda miundombinu tukuhudumie ikiambatana na utoaji wa miundombinu ya umeme katika kuilinda ambapo amesema kampeni hiyo ni endeleo itaanza leo na itadumu kwa miezi sita.
“Lengo la kampeni yetu kwanza ni pamoja na kuhamasisha ulipaji wa madeni kama unavyofahamu tuna wateja wa aina mbili wa kwanza ni wateja wanaolipa kwanza na wale wanaotumia umeme na kulipa baada sasa tunayo changamoto ya uwepo wa madeni ya wateja wa malipo ya baada kwa maaana ya wateja wakubwa na wateja wa kati ambayo tumeona ni vyema tukitumia fursa hii kuweza kuwakumbusha wateja wetu wote nchi nzima kulipa umeme kwenye bili zao kwa hiari kwa sababu kumekuwa na malimbikizo ya madeni .
“Hivyo kama Shirika madeni haya yanatupa changamoto kuendesha shughuli zetu kwa hiyo tukaona ni wakati mzuri wa kuweza kuwakumbusha wateja wa malipo ya baada kuweza kulipa bili zao za ankara za umeme,”amesema Irene.

Ameongeza kuwa katika kampeni hiyo, TANESCO imetoa dirisha la msamaha wa riba kwa muda wa miezi sita, ili kuwapa nafasi wadaiwa kulipa madeni yao kwa urahisi zaidi.
“Msamaha huu ni wa muda, lakini ni hatua endelevu. Tunatoa nafasi ya miaka kumi kwa wateja waliokumbwa na madeni ya muda mrefu kushughulikia malimbikizo yao kwa maelewano,” amesema.