Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imekuja na mbinu ya kudhibiti mikopo umiza kwa Watanzania kwa kuzitaka taasisi zote ndogo za fedha daraja la pili 2600 kujisajili katika vyama vya Umoja wa watoa huduma ndogo za fedha Tanzania(TAMIU) na Taasisi ya Umoja wa Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha(TAMFI) ndani ya miezi sita.

Taasisi isiyojisajili hadi Desemba, mwaka huu itanyang’anywa leseni na BoT, lengo likiwa kuhakikisha zinatoa huduma nzuri kwa walaji na kuondoa changamoto kwa jamii.
Kauli hiyo ilitolewa leo na jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT, Emanuel Tutuba katika uzinduzi wa utaratibu wa usimamizi binafsi kwa taasisi za huduma ndogo za fedha za daraja la pili kati ya BoT na Vyama vya watoa huduma ndogo za fedha.
“Utekelezaji huu mpya tuliingia makubaliano ya usimamizi binafsi wa sekta ndogo ya fedha Machi, mwaka huu, kati ya BoT na vyama vya taasisi za huduma ndogo za fedha viwili ,tumeingia makubaliano ikiwa ni hatua mojawapo ya kuongeza jitihada za pamoja, kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara, kuleta mshikamano na kuiwezesha sekta hii ya fedha kuwa nzuri.
“Mtakumbuka palikuwepo na majina mabaya kwa watoa huduma wa sekta hii ndogo ya fedha, majina yale inaonekana yalitokea kutokana na huduma zilizokuwa zikitolewa ambayo ni mikopo umiza, mikopo ya kausha damu, mikopo ya kaba roho,”ameeleza.

Amesema hatua hiyo waliyoizindua ni sehemu ya juhudi za pamoja kuweka mazingira rafiki, kisera kisheria na kitaasisi kwa sekta ndogo za fedha nchi iliyoendelea kukua kwa kasi kubwa na hadi sasa zipo taasisi 2600.
Tutuba alisema jinsi ya kuzifikia wakaona utaratibu huo wa kujisimamia wenyewe wa kufuata misingi ya masharti yaliyopo katika leseni zao itakuwa ni fursa za kuwawezesha watoe huduma nzuri na kuendelea kuwalinda wateja wao na watu wanaopata huduma za fedha kupata kwa viwango vinavyostahiki bila kubugudhiwa na watoaji kutoa kwa viwango vinavyotakiwa.
“Tukio hili litaendelea kutoa huduma chanya na jumuishi kwa huduma za fedha nchini hasa kwa wananchi wa kipato cha chini na wajasiriamali wadogo ambao wamekuwa ndio wateja wakubwa wa kutafuta fedha katika taasisi hizo za daraja la pili,”amesema.

Amesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la watoa huduma ndogo za fedha nchini hivyo BoT itahakikisha inajenga nidhamu nzuri ya soko kutoa huduma zisizoumiza Watanzania.
Gavana Tutuba amezitaka taasisi zinazofanya biashara ya kukopesha fedha bila leseni kuacha mara moja kwa sababu ni kosa kisheria kukopesha fedha bila leseni ya BoT kwa daraja la pili hivyo mtu ahakikishe anapata huduma za kifedha kwa taasisi ziliyosajiliwa.
Tutuba ameshauri mtu anapokwenda kukopa asome mashatri na viwango vya riba hivyo taasisi zitakazokiuka masharti zitafutwa na mwaka jana 58 zilifutwa hivyo BoT itaendelea kuzifuatilia taasisi hizo kwa ukaribu kuondoa malalamiko kwa Watanzania.
Amesema kupitia utaratibu uliozinduliwa BoT itaendelea kuwa na utekelezaji mzuri wa usimamizi binafsi kwani ni nyenzo muhimu kuufikia malengo ya taifa ya kuboresha huduma jumuishi za kifedha .

Pia Tutuba alisema kiwango cha upatikanaji wa huduma rasmi za fedha nchini bado kiko chini, kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2023 kiwango kilikuwa asilimia 76.
“Tulijiwekea lengo la kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2028 lakini kwa kasi na ushirikiano tunaouna tutavuka lengo, kwa uwekezaji uliofanywa na serikali naamini mifumo ya kidigitali imekuwa chachu ya watu kutoa huduma hizo,” amrsema.
Amesema ushirikiano wa benki namna zinavyofanya kazi zimekuwa chachu ya watumia wa huduma mijini na pembezoni na mifumo ya kidigitali kwa kampuni za simu zimekuwa na ubunifu kupeleka huduma kwa wananchi.
Amewataka wananchi kutumia huduma za fedha mtandaoni kukuza uchumi na kuboresha maisha kwa ujumla na watoa huduma kuongeza kasi ya elimu ya kifedha nchini.

Naye Mkurugenzi wa Sekta ya Fedha BoT, Sadat Musa amesema hatua hiyo ya kuimarisha mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha itakuza uchumi na kuongeza ujumuishi wa huduma za fedha nchini
Amesema vyama hivyo viwili vimekidhi na kubeba dhamana ya kanuni maadili za watoa huduma ndogo za fedha hiyo ni njia fanisi kujenga sekta ya fedha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TAMFI, Devotha Minzi amesema watekeleza yale waliokubaliana ili kujenga na kuboresha huduma huduma ndogo za fedha na huduma bora kwa walaji.