Na Mwandishi wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza kampuni ya Royal Suites Of Zanzibar Company Limited, inayomilikiwa na familia ya Raza Mohamed Hassan, kwa uamuzi wao wa kizalendo kuwekeza katika hoteli ya kisasa yenye hadhi ya nyota tano, kwa lengo la kutoa huduma bora za mikutano na malazi kwa wageni wa kimataifa na wageni mbalimbali wanaotembelea Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Julai, 12 2025, katika hafla ya Uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Hoteli ya Golden Tulip Airport, iliyofanyika Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema kuwa kukamilika kwa awamu ya pili ya ujenzi wa hoteli hiyo ni ushahidi tosha wa mafanikio ya sera za Serikali katika kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji na ustawi wa sekta ya utalii Zanzibar.

Amesema kuwa mradi huo ulisajiliwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) mnamo tarehe 31 Disemba 2015, ukiwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 8 kwa awamu ya kwanza, hadi hivi sasa kufikia uwekezaji wa jumla wa Dola milioni 14.
“Mazingira bora ya biashara, sera imara za uwekezaji, na maendeleo ya miundombinu vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia wawekezaji wa ndani kuendelea kuwekeza,”amesema.
Ameeleza kuwa Serikali imeboresha na kurahisisha taratibu za usajili kwa kutumia mfumo wa “One Stop Centre” ndani ya ZIPA, ambapo cheti cha uwekezaji hutolewa ndani ya saa 24 baada ya taratibu kukamilika.

Rais Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kuwa miradi ya uwekezaji ina manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi kupitia ajira, matumizi ya rasilimali za ndani, na kukuza utalii endelevu.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wawekezaji pamoja na wageni waalikwa mbalimbali.