Home KITAIFA TANESCO yaandika historia ajira mpya

TANESCO yaandika historia ajira mpya

📍Waajiriwa wapya 555 wapata ajira kwa mara moja

📍Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO afungua rasmi mafunzo elekezi kwa waajiriwa hao

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeandika historia kwa kuajiri watumishi wapya 555 kwa mara moja, hayo yameelezwa katika uzinduzi wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa hao.

Mafunzo hayo yamefunguliwa Julai, 21 2025 jijini Dodoma Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dk. Rhimo Nyansaho yakilenga kuwapa uelewa mpana kuhusu majukumu yao ndani ya Utumishi wa Umma na ndani ya Shirika, kabla ya kuanza kazi rasmi katika maeneo waliyopangiwa kote nchini.

Akifungua mafunzo hayo, Dk. Nyansaho aliwataka watumishi hao wapya kutambua uzito wa fursa waliyoipata na kuitumikia kwa bidii, uadilifu, na uaminifu mkubwa.

“Kipekee namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kibali cha kuajiri. Hii ni fursa ya kipekee, na ni wajibu wenu kuithamini kwa kufanya kazi kwa juhudi na weledi mkubwa,” amesisitiza Dk. Nyansaho.

Amewaasa kuhusu mwenendo wao wa kikazi, aliwakumbusha kuwa TANESCO imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma bora kwa wateja, hivyo wanapaswa kuendeleza juhudi hizo kwa kuwahudumia wateja kwa kuwajibika na kuwa na maadili ya hali ya juu.

“Tumepiga hatua kwenye utoaji wa huduma bora kwa wateja, hivyo ni muhimu muiendeleze kwa kuwahudumia wateja kwa uaminifu na uadilifu kwa maslahi mapana ya Shirika na Taifa kwa ujumla” mesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, aliwataka waajiriwa hao kuwa mabalozi wa Shirika katika maeneo yao ya kazi kwa kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uaminifu, na kwa kutoa huduma bora kwa wateja.

“Katika majukumu yenu, mnakwenda kukutana na wateja wetu. Wahudumieni kwa heshima na kwa moyo wa kujitolea, ili kwa pamoja tuendelee kujenga taswira chanya ya TANESCO,” ameeleza Twange.

Waajiriwa hao wameajiriwa na TANESCO hivi karibuni baada ya kupitia mchakato wa ajira, huku awali wakiwa wafanyakazi wa mikataba ya muda na ajira hizi mpya zinawapa fursa ya kupata ajira za kudumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here