Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa(TAMISEMI) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wameandaa shindano la insha ikiwa ni kuelekea kumbukizi ya miaka 26 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai,22 2025 Jijini Dar es salaam jana Mkurugenzi wa Huduma za Televisheni wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Happiness Ngasala, amesema lengo la shindano hilo la insha ni kumuenzi Hayati Mwalimu Nyerere kwa mambo mazuri aliyoyafanya katika uhai wake.
“Katika kumbukizi ya miaka 26 ya kifo Cha baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere tumeamua kuandaa shindano hili ambalo litausisha wanafunzi kutoka shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita watayaekeza mambo mbalimbali aliyoyafanya Hayati Mwalimu Nyerere kupitia mfumo wa Isha kupitia mada ya maadui watatu ambao ni ujinga,maradhi na umasikini,” amesema Ngasala.
Asema shindano la insha ya Mwalimu Nyerere limeanza rasmi Julai 22 ,mwaka huu na linatarajia kuhitimishwa Octoba 14,mwaka huu ,huku likibebwa na mada ya maadui watu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini mambo ambayo yalishika hatamu katika Uongozi wake.

Amesema washindi watano katika shindano hilo watapewa zawadi za mbalimbali ikiwemo kompyuta mpakato, vyeti pamoja na fedha taslimu.
“Ili kutokomeza ujinga mageuzi ya elimu yaliofanyika na Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa elimu yetu lazima ijenge moyo wa kujitokeza kwa jamii nzima na kuwasaidia wanafunzi kukubali mabadiliko yanayoendana na maisha yetu badala ya yale ya kikoloni”amesema
Akizungumzia maandalizi alisema yamekamilika na mada ya shindano hilo zitasambazwa katika shule zote za Tanzania Bara na Visiwani .
Ametoa wito kwa wanafunzi kushiriki katika shindano hilo huku akiwataka washiriki kutokutumia udanganyifu au akili unde (AI) na kueleza watakaofanya hivyo watagunduliwa na kuondolewa katika shindano hilo.

Katika hatua nyingine Ngasala amesema mbali na uandishi wa Insha kwa wanafunzi pia TBC imeandaa mbio zitazojulikana kama Mwalimu Nyerere Marathon zitakazofanyika Oktoba 14,mwaka huu Mkoani Mbeya.Pia katika Kilele hicho kutakuwa na wiki ya vijana ambayo itausisha shughuli mbalimbali.