Na Mwandishi wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, ameungana na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini kushiriki hafla ya uzinduzi wa Ratiba ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara, kwa mwaka 2025.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Julai 26, 2025, katika ofisi za Makao Makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jijini Dodoma, na umeongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele.
Tukio hili limeelezwa na viongozi mbalimbali kuwa ni hatua muhimu katika kuelekea uchaguzi mkuu ujao, na linaakisi dhamira ya Tume ya Uchaguzi kuhakikisha maandalizi ya uchaguzi yanatekelezwa kwa uwazi, ushirikishwaji na kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Katibu Mkuu wa NLD, Doyo, ameeleza kuwa chama chake kipo tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Oktober mwaka huu. Alisema kuwa chama kimejipanga kusimamisha wagombea wa udiwani na ubunge katika majimbo na kata zote nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha sauti za Watanzania kutoka kila pembe ya nchi zinasikika kupitia chama cha National League for Democracy.
“Kwa sasa tumeshakamilisha asilimia 85 ya zoezi la ndani la uteuzi na uhakiki wa wagombea wetu, na matarajio yetu ni kuhakikisha tunafikia asilimia 100 kabla ya muda wa uteuzi rasmi kuanza,” amesema.
Ameongeza kuwa chama chake kinasimamia misingi ya uzalendo, haki, maendeleo na usawa jumuishi, na kimejipanga kutoa sera mbadala zinazolenga kuinua maisha ya wananchi wa Tanzania.
Chama cha NLD kimeahidi kuendesha kampeni safi, ya kistaarabu na inayojikita katika hoja na sera, huku kikitoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi kuheshimu sheria, taratibu, na misingi ya demokrasia.